Kwa mara ya kwanza Rais wa shirikisho la soka duniani (FIFA) Gianni Infantino amekutana na Rais wa Marekani Donald Trump katika ofisi ya Oval na kujadili masuala ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2026, ambazo zitaandaliwa kwa ushirikiano wa nchi za Marekani Canada na Mexico.

Kabla ya mazungumzo ya viongozi hao, waandishi wa habari walipata nafasi ya kupiga picha tukio la iInfantino kumkabidhi jezi Trump yenye namba 26, ambayo inaaminisha mwaka ambao nchi yake itashiriki kuandaa fainali za kombe la dunia, pamoja na kadi nyekudu na manjano.

Tukio hilo lilionekana kumfurahisha Trump ambaye alikua mwenye furaha.

Hata hivyo Infantino alitumia nafasi ya kumkabidhi kadi rais huyo wa Marekani, kwa kumtania, ambapo alisema: “Mheshimiwa unaweza kutumia kadi hizi katika mikutano yako na waandishi wa habari.”

Katika hatua nyingine Rais wa FIFA alimwambia Trump kuwa, anaamini Marekani kuwa sehemu ya wenyeji wa fainali za mwaka 2026, italeta tija kubwa kwa timu zitakazopata nafasi kushiriki kwa mwaka huo, kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoefu wa mwaka 1994, ambapo walikua wenyeji kwa mara ya kwanza.

Kwa upande wa Trump alisema, amefarijika kukutana na kiongozi wa soka duniani, na akamuhakikishia maandalizi ya fainali za kombe la dunia 2026 yatakua mazuri kwa nchi yake, sambamba na nchi jirani.

‘Nimefarijika sana kukutana na wewe, nikuhakikishie kwamba mwaka 2026 mambo yatakua mazuri, ninauhakika zitakua fainali zenye mvuto kuliko za miaka ya nyuma.

Wakati huo huo Trump akampongeza Infantino, kwa juhudi zake za kuhakikisha rushwa inamalizwa katika mchezo wa soka, akitumia mfano wa sakata lililomfika aliyekua Rais wa FIFA Sepp Blatter na genge lake, ambao kwa pamoja waliadhibiwa.

‘Soka ni mchezo unaokusanya hisia za watu wengi duniani, ninakupongeza sana kwa kuonyesha ukakamavu katika kupiga vita suala la rushwa katika mchezo huu, viongozi waliopita wameadhibiwa ukiwa tayari umeshaingia madarakani, ninakuhakikishia katika hilo tupo pamoja na ukihitaji msaada wangu nitakuwa radhi kujitoa kwa asilimi 100.”

Kenya Yajitoa kuandaa michuano ya CECAFA 2018
Video: Bahati nzuri kwangu sijafa, bahati mbaya sana kwao sijafa- Tundu Lissu