Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee,  Dk. Hamisi Kigwangalla jana aliwasimamishwa kazi wauguzi wa zamu katika hospitali  ya  Temeke jijini Dar es Salaam kwa kosa la kufanya biashara ya kuwauzia wagonjwa gloves na nyuzi za kushonea vidonda kwa bei ya juu na wengine kwa tuhuma za kupokea rushwa.

Dk. Kigwangalla alichukua uamuzi huo baada ya kupata malalamiko na shuhuda za watu mbalimbali waliofika katika hospitali hiyo wakiwa na wagonjwa wao hususan wanawake katika wodi ya wazazi.

Mmoja kati ya wananchi waliotoa malalamiko yao alimwambia Dk. Kigwangalla kuwa alilazimika kununua gloves kwa muuguzi mmoja wa zamu kwa shilingi 5,000 ili mgonjwa wake apate matibabu, ili hali gloves hizo zinapatikana maduka ya nje kwa shilingi 1,000 tu.

Kufuatia sakata hilo, Dk. Kigwangalla aliamuru wauguzi wote waliokuwa zamu usiku wa kuamkia jana kusimamishwa kazi mara moja kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

“Nimewasimamisha kazi wauguzi wote waliokuwa zamu jana (juzi) asubuhi, nakuagiza Msajili wa Baraza la Wauguzi uwasimamishe hadi utakapowasafisha kupitia kamati ya msajili,” alisema.

Kadhalika, aliwasimamisha kazi wauguzi wengine sita kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa na kuagiza Takukuru kuwachunguza.

Wauguzi hao waliosimamishwa kwa tuhuma za rushwa ni Hadija Salum, Beatrice Temba, Agnes Mwampashe, Elizabeth Mwilawa, Mariam Mohamed na Marion Said, ambao walikuwa zamu katika wodi ya wajawazito wakati wa tukio hilo.

‘Paul Makonda Amewatonesha walimu vidonda’
Polisi wapekua Nyumba ya Halima Mdee, watoka na hili