Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Didier Gomes, amemshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo Mohamed Dewji (Mo) na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez kwa ushirikiano waliompa hadi kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jana Jumapili (Julai 11).

Gomes amesema uongozi wa klabu ya Simba SC ukiongozwa na viongozi hao walimuamini na kumpa ushirikiano mkubwa na ndiyo sababu iliyotufanya kutwaa ubingwa wakiwa na michezo miwili mkononi.

Gomes amesema hawezi kuwa kocha bora bila kuwa na wachezaji bora hivyo amekimwagia sifa kikosi chake kwa uimara wake huku akisema wamestahili kutwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.

Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema msimu huu kikosi chake kimekuwa bora na kimestahili kutwaa ubingwa kwa sababu ndiyo timu iliyofunga mabao mengi na kufungwa machache kuliko timu zote zilizoshiriki Ligi Kuu.

“Lazima tumshukuru Mwenyekiti wa Bodi na CEO Barbara kwa ushirikiano walionipa kwanza kuniamini naweza kuifundisha hii timu na kuipa mafanikio. Pia siwezi kuacha kuwataja wachezaji wangu kwenye ubingwa huu, huwezi kuwa kocha bora bila kuwa na wachezaji bora pia tulikuwa na kikosi imara.”

“Tumestahili kuwa mabingwa msimu tulikuwa bora zaidi ya timu zote,” amesema Gomes.

Simba SC imebakisha michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC na Namungo FC pamoja na mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Young Africans utakaochezwa Julai 25, mkoani Kigoma.

Hii ndo suluhu ya ajali za barabarani
Lamine Moro mambo safi Young Africans