Baada ya kupisha michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022, Kocha Mkuu Simba SC Didier Gomes wamewataka wachezaji Peter Banda na Duncan Nyoni kureja Tanzania haraka, tayari kwa safari ya kuelekea Botswana.

Simba SC inatarajiwa kusafiri hadi mjini Gaborone, Botswana kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy utakaochezwa Oktoba 17, kisha itacheza mchezo wa Mkondo wa Pili jijini Dar es salaam Oktoba 22.

Kocha Gomes amewaagiza wachezaji wote ambao wapo kwenye majukumu ya timu za Taifa, kuripoti mapema kambini mara tu baada ya kumaliza majukumu hayo, ili kujiandaa na mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa.

Gomes amesema kikosi chake kinaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo huo, na ana matarajio makubwa ya kupambana na kushinda ugeni na nyumbani.

Amesema mpaka sasa baadhi ya wachezaji wake hawajafika kambini kuungana na wenzao kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy, lakini ameutaka Uongozi kuhakikisha wanafika kwa wakati ili kukamilisha maandalizi ya wachezaji wenzao.

“Kikosi chetu kinaendelea vizuri na maandalizi za mchezo wetu wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy, tunajua utakuwa mchezo mgumu hasa kutokana na ubora wa wapinzani wetu, ambao walianzia hatua ya awali ya michuano hiyo na kufuzu kwa ushindi mkubwa.

“Changamoto tuliyonayo ni ile ya baadhi ya nyota wetu muhimu kuwa katika majukumu ya timu zao za taifa, lakini tayari nimewasiliana na Uongozi kwa ajili ya kuhakikisha wachezaji wote ambao wapo katika majukumu ya timu zao za Taifa wanaripoti kambini haraka inavyowezekana, ili tupate muda wa kujiandaa na mchezo dhidi ya Galaxy.”

Mshindi wa Jumla wa mchezo huo atatinga hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku atakayepoteza atashuka kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na kucheza michezo ya mtoano kabla ya kutinga hatua ya Makundi.

Biashara United yasaka fedha za nauli ya Libya
Mfikirwa afichua mpango Young Africans