Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes amewataka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kuwasahau wachezaji Luis Miquissone na Clatous Chama, ambao waliuzwa wakati wa dirisha kubwa la usajili 2021/22.

Chama aliondoka Simba SC baada ya kuuzwa kwenye klabu ya RS Berkane ya Morocco huku Luis Miquissone akiuzwa kwa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly ya Misri.

Kocha Gomes amesema kuna haja ya kila Shabiki na Mwanachama wa Simba SC kujenga mazoea ya kuwaamini wachezaji waliopo kikosini kwa sasa, huku akisisitiza wawasahau wachezaji hao wawili, ambao wanatajwa kuwa msaada mkubwa katika kutwaa mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa misimu miwili iliyopita.

“Nawashangaa sana wanaoendelea kuwataja Luis na Chama wakati hawapo sasa, tuna wachezaji wapya na wao pia wana uwezo japo wanahitaji muda ili kuingia kwenye mfumo, hao wanaowataja sasa walipokuwa wanaingia mara ya kwanza Simba hawakuwa na ubora huo walioondoka nao.”

“Kila mchezaji ana aina yake ya uchezaji na ana umuhimu wake, pia akina luis walikuwepo walicheza vizuri na sasa wameondoka. kuondoka kwao sio kwamba wameondoka na timu wameiacha na itaendelea kufanya vizuri kwani imesajili mbadala wao na sasa tunahitaji kuwapa muda na kuwaamini na bila shaka wataleta matokeo chanya.” amesema Kocha Didier Gomes.

Kuondoka kwa Luis Miquissone na Clatous Chama, kulitoa nafasi ya kusajiliwa kwa wachezaji wengine ndani ya kikosi cha Simba SC kama Peter Banda, Duncan Nyoni, Pappe Oussmane Sakho na Henock Enonga.

Mayele awatuliza mashabiki Young Africans
Kim Jong Un ailaumu Marekani kwa kusababisha wasiwasi kwenye rasi ya Korea