Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, watacheza mchezo wa kwanza wa kimataifa wa kirafiki Jumamosi (Agosti 21), wakiwa nchini Morocco walipoweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Taarifa kutoka Simba SC zimeeleza kuwa Mabingwa hao watacheza dhidi ya FAR Rabat ya nchini Morocco, inayonolewa na kocha wao wa zamani Sven Vandebroeck.

Mchezo huo utakua wa kwanza kwa makocha Didier Gomes na Sven Vandebroeck kukutana kimajukumu, na unatarajiwa kuwa na changamoto za kujifunza mambo mengi kuelekea msimu mpya wa 2021/22.

Hata hivyo Kocha Gomes amekiri kwamba kikosi chake kinazidi kuimarika kadri mazoezi yanavyochanganya huko nchini Morocco, hivyo mchezo dhidi ya FAR Rabat utakua kipimo kizuri kwa wachezaji wake wote.

Kocha Sven ndiye aliepelekea Simba SC hatua ya Makundi msimu uliopita na kisha aliondoka klabuni hapo na kutimkia FAR Rabat, huku Gomez akirithi mikoba yake na kufanikiwa kuivusha timu hiyo hadi hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Msimu wa 2019/20 Kocha Sven, aliiwezesha Simba SC kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho (ASFC), halikadhalia Gomez amefanya hivyo kwa msimu wa 2020/21.

Serikali yazidi kuboresha sekta ya Afya
Sabaya amkana msaidizi wake, atiririka ‘siri’ akijibu maswali