Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, leo jioni wataendelea na mchakato wa kutetea taji lao kwa kucheza dhidi ya Biashara United Mara, Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, mjini Musoma mkoani Mara.

Simba SC iliwasili mjini Musoma jana asubuhi ikitokea jijini Mwanza, na jioni ilifanya mazoezi yake ya mwisho kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume.

Kocha mkuu wa Simba SC Didier Gomes, amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo, ambao anaamini utakua mgumu na mazuri kwa pande zote mbili.

“Ninawatambua Biashara United ni moja ya timu bora na imara ikiwa ndani ya uwanja kwa namna ambavyo inacheza na kutafuta ushindi.”

“Wanacheza vizuri hilo lipo wazi ila ninaona nami kikosi chetu kipo imara hasa baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wetu wa AS Vita nchini DR Congo jambo ambalo linatuongezea nguvu ya kujiamini.” Amesema kocha huyo kutoka nchini Ufaransa.

Kwa upande wa kocha wa Biashara United Mara Francis Baraza, amesema wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo na wanahitaji kupata alama tatu kwenye uwanja wa nyumbani.

“Hitaji letu ni alama tatu tukiwa nyumbani hapa Musoma, nina imani maandalizi tuliofanya yanatosha kuwakabili Simba SC na kufanikisha lengo la kuwafurahisha mashabiki wetu.” Amesema Baraza

Kocha huyo ameweka wazi kuwa wachezaji wake wote wana nafasi sawa ndani ya uwanja hivyo hakuna mwenye namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza hivyo kunaweza kuwa na mabadiliko kikosi cha kwanza.

“Kila mchezaji wangu ana nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza, hivyo itafahamika nani na nani ataanza kwenye mchezo wetu wa leo, ambao nina imani kubwa tunakwenda kufanya vizuri.” Aliongeza Baraza.

Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 39 imeachwa kwa jumla ya alama 7 na watani zao wa jadi Young Africans ambao wapo nafasi ya kwanza na alama 46.

Young Africans imecheza jumla ya michezo 20 huku Simba ikiwa imecheza jumla ya mechi 17 kwa msimu wa 2020/21 ambao umekuwa na ushindani mkubwa.

Azam FC kujiuliza kwa Mbeya City leo
Kaze aukubali 'MZIKI' wa Kagera Sugar, Mexime achekelea