Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bw.Godwin Gondwe amepiga marufuku wananchi wa wilaya yake kucheza mchezo wa bao na “pool table” wakati wa mchana muda ambao ni wa kufanya kazi ili kutekeleza falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya “Hapa kazi Tu”.

Gondwe alitoa kauli hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mambo mbalimbali yanayohusu wilaya yake ya Handeni ambapo alisema katika wilaya hiyo baadhi ya vijana hawana muamko wa kufanya kazi badala yake wamekua wakijishughulisha na kucheza bao na “pool table” vitu ambavyo haviwaletei maendeleo.

“Nimekataza vijana katika wilaya yangu kucheza michezo ya bao na “pool table” wakati wa kazi na nimewahamasisha kushiriki shughuli za ufugaji na kilimo kwa ajili ya kujiletea maendeleo na kuondokana na hali ya umasikini” alisema Gondwe.

Mkuu huyo wa Wilaya aliwashauri wakazi wa Handeni kujishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali ya biashara  ikiwemo alizeti, ufuta na ufugaji wa mbuzi na kuku ili waweze kujipatia fedha zitakazowasaidia kujikimu kimaisha.

Pia Gondwe alisema kuwa wamekubaliana na Idara ya Ardhi wilayani humo kutenga maeneo maalum ya uwekezaji kwa vijana ambapo Serikali itawawezesha kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kilimo.

Amewataka vijana kujiunga katika vikundi waweze kupatiwa fedha ambazo kila Halmashauri imetenga kwa ajili ya vijana na wanawake na watumie mikopo hiyo  kujikwamua kimaisha kwa kufanya shughuli za ujasiliamali.

Akizungumzia tatizo la ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo, Gondwe alisema bado anaendelea kushirikiana na  wadau mbalimbali kuhakikisha tatizo la maji wilayani Handeni linapungua ili wananchi waweze kuondokana na adha hiyo ambayo inawakabili kwa muda mrefu.

Alisema wananchi wa Handeni hasa wanawake wanapata tabu ya kutafuta maji safi na salama ingawa Serikali bado inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma hiyo kwa uhakika

Video: Wizara Ya Maliasili Na Utalii Kuchangia Ukuaji Wa Pato La Taifa
Wizara Ya Maliasili Na Utalii Kuchangia Pato La Taifa