Wachezaji wa Gor Mahia FC ya Kenya jana Jumapili (Februari 21) baada ya mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup) dhidi ya Napsa Stars ya Zambia, kumalizika walimshambulia mwamuzi wa mchezo huo.

Pamoja na hilo wachezaji hao pia waliharibu vitu vya thamani kwenye vyumba vya kubadilisha nguo katika uwanja wa Heroes, ambao ulishuhudia wawakilishi hao wa Kenya wakitupwa nje ya michuano hiyo.

Hata hivyo Shirikisho la soka Barani Afrika CAF bado halijatoa kauli yoyote kuhusu vurugu hizo, lakini linatarajiwa wakati wowote tamko kutoka kwenye shirikisho hilo litasambazwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Endapo itathibitika wachezaji wa Gor Mahia walimpiga mwamuzi wa mchezo huo, kuna hatari ya kufungiwa mchezo mmoja mmoja ama timu nzima kwa ujumla kushiriki michuano ya kimataifa, sambamba na kutozwa faini.

Timu hizo katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa nchini Kenya Napsa ilishinda kwa bao moja kwa sifuri na jana Jumapili Gor Mahia iliondoka asubuhi kwenda Zambia kwa ajili ya mchezo wa marudiano na ilifika nchini Zambia saa mbili kabla ya mchezo huo ambao walitoa sare ya mabao 2-2, huku wenyeji Napsa wakisawazisha dakika ya 90 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-2.

Kwa matokeo hayo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ni Tanzania pekee iliyosalia na wawakilishi katika michuano ya kimataifa, wakiwakilishwa na mabingwa wa Ligi Kuu Simba SC kwenye michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika.

Upande wa Kombe la Shirikisho Tanzania inawakilishw ana Namungo FC ambayo inaongoza kwa mabao 6-2 dhidi ya Clube Desportivo 1º de Agosto ya Angola, huku ikisubiri mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa juma hili jijini Dar es salaam, Tanzania.

Kituo cha mabasi Mbezi Louis kuanza kazi Feb. 25
Majaliwa awakabidhi magari polisi Lindi