Kiungo kutoka nchini Brazil José Paulo Bezerra Maciel Júnior (Paulinho) ameondoka FC Barcelona na kurejea nchini China kwenye klabu ya Guangzhou Evergrande, kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja akitokea kwa mabingwa wa soka Hispania, FC Barcelona.

Klabu ya Guangzhou iliyokuwa ikimmiliki kiungo huyo kabla ya kutua FC Barcelona msimu uliopita, imeripotiwa kukamilisha mpango huo kwa kutoa Euro milioni 50, sawa na Pauni milioni 44.2m, huku FC Barcelona wakitengeneza faida ya Pauni milioni 4.

Msimu uliopita FC Barcelona walimsajili kiungo huyo kwa ada ya Pauni milioni 40.

Guangzhou Evergrande tayari wameshatangaza kurudi kwa Paulinho kupitia vyanzo vyao vya habari, na wanaamini uwepo wake kwa mara nyingine tena utawasaidia kufanya vyema msimu ujao wa ligi.

“Mfalme amerudi,” ni ujumbe ulioandikwa katika vyanzo mbalimbali vya habari vya klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu nchini China.

Kabla ya kuondoka Guangzhou msimu uliopita, kiungo huyo alikuwa ameshacheza michezo 84 na kuifungia klabu hiyo mabao 22.

Akiwa FC Barcelona msimu uliopita Paulinho alikuwa miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi cha kwanza, na alifanikiwa kufunga mabao tisa katika michezo 49 aliyocheza.

Misimu saba iyopita klabu ya Guangzhou Evergrande ilitamba kwa kuwa bingwa wa ligi ya china, lakini kuondoka kwa Paulinho msimu uliopita kuliwasababishia kuukosa ubingwa na kujikuta wakimaliza katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Chinese Super League.

Paulinho alisajiliwa na Guangzhou Evergrande mwaka 2015 akitokea Tottenham Hotspur ya England, ambapo huko alicheza michezo 45 na kufunga mabao 6.

Jose Francisco Molina amrithi Fernando Hierro
Lucas Torreira kumalizana na Arsenal