Klabu ya Valencia inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Hispania (La Liga), imekamilisha mpango wa kumsajili jumla mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Ureno Gonçalo Manuel Ganchinho Guedes, akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG), kwa ada ya Euro milioni 40.

Mmiliki wa klabu ya Valencia yenye maskani yake makuu Mestella Stadium mjini Valencia, Peter Lim, amefanikisha usajili wa mshambuliaji huyo kwa kutumia ukaribu wake na mmiliki wa mabingwa wa soka nchini Ufaransa  Nasser Al Khelaifi.

Wakala wa mshambuliaji huyo Jorge Mendes alikua kichocheo kikubwa cha kuhakikisha Guedes anaondoka jumla PSG, baada ya kutumika kwa mkopo msimu uliopita akiwa na Valencia.

Kabla ya fainali za kombe la dunia zilizochezwa nchini Urusi mwaka huu, Valencia waliwasilisha ofa ya Euro Milioni 40, lakini zilikataliwa kwa kisingizio cha uongozi wa PSG kuwa kwenye mchakato wa kumsaka meneja mpya, baada ya kuondoka kwa Unai Emery.

Hata hivyo viongozi wa Valencia hawakukata tamaa, na kwa mara kadhaa walikutana na mkurugenzi wa michezo wa PSG Antero Henrique, hadi walipofanikisha lengo la kumsajili moja kwa moja Guedes mwenye umri wa miaka 21.

Meneja wa Valencia Marcelino García Toral alitoa kipaumbele cha kuushawishi uongozi wake ili kuhakikisha Guedes anasajili jumla klabuni hapo, baada ya kuridhishwa na uwezo wake msimu uliopita. Mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga mabao matano katika michezo 33 ya ligi aliyocheza.

Usain Bolt kujaribiwa Central Coast Mariners
Hawa Ghasia ajiuzulu nafasi yake CCM