Aliyekua meneja wa muda wa vinara wa ligi kuu ya soka nchini England (Chelsea) Guus Hiddink amekataa ombi la uongozi wa klabu ya Leicester City la kutaka awe mbadala wa Claudio Ranieri.

Ranieri raia wa nchini Italia, alitimuliwa King Power Stadium mwezi Februari, kufuatia mambo kumuendea kombo katika harakati za kutetea taji la ligi ya England.

Hiddink aliamiwa na viongozi wa Leicester City huenda angefaa kushika madaraka ya ukuu wa benchi la ufundi la klabu hiyo, kutokana na umahiri wa ufundishaji wake pamoja na kuifahamu vyema ligi ya nchini England.

Hiddink ambaye aliwahi kuinoa timu ya taifa ya Uholanzi kwa vipindi tofauti, amethibitisha kutokua tayari kurejea nchini England alipohojiwa na gazeti la Sunday Times, ambalo lilihitaji kufahamu msimamo wake kufuatia ombi la viongozi wa Leicester City ambalo liliwasilishwa kwake mapema mwezi uliopita.

Mdachi huyo aliliambia gazeti hilo kuwa “Bado sijafanya maamuzi yoyote mpaka sasa, na viongozi wa Leicester hawajaonyesha utayari wa kufanya kazi na mimi, hawajazungumza wazi kuhusu ombi lao. Lakini natambua umuhimu wa kuhitajika kwa meneja ndani ya klabu hiyo…’

“Wamenifuata mara kadhaa, lakini hawajaweka wazi nini wanachokihitaji kwangu zaidi ya kuniomba niwe meneja wa kikosi chao, mimi ni mtu ambaye ninajua taratibu za ajira, ninatakiwa kujua kila hatua nitakayopitia, siwezi kukubali kwa ombi ambalo limefichwa.

“Bado ninaamini meneja wa muda Shakespeare anaifahamu vizuri klabu, ninawashauri waendelee kufanya nae kazi, na matokeo mazuri yataendelea kupatikana, hundo ndio ushauri na msimamo wangu dhidi ya viongozi wa Leicester City.” Alisema Hiddink.

Craig Shakespeare, ambaye alikuwa meneja msaidizi wakati wa utawala wa Claudio Ranieli, amekua na bahati ya kupata matokeo mazuri tangu alipokabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi kwa muda, na mpaka sasa ameshakiongoza kikosi cha Leicester City katika michezo kadhaa na kupata ushindi.

Tangu Shakespeare alipokabidhiwa jukumu la kuwa meneja wa muda Leicester City wameifunga Liverpool (3-1), Hull City (3-1), Sevilla (2-0), West Ham (3-2) na Stoke City (2-0).

Zanzibar kuimarisha uchumi kupitia wasomi
Video: CCM kuanza mikakati ya ushindi 2020