Mbunge wa Kawe ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amejibu kuhusu uwepo wa kikosi kinachoitwa ‘Sukuma Gang’, ambacho kinadaiwa kuwa na nia ya kumkwamisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Akijibu swali la mwandishi wa habari ambaye alitaka kupata majibu kutoka kwa kiongozi huyo akieleza kuwa inaaminika yeye ndiye kiongozi wa kundi hilo, Gwajima alikana na kutoa sababu za kutohusika.

“Wanauliza kwamba kulikuwa na ‘Sukuma Gang’ ambayo kazi yake ni kumharibia Rais Samia Suluhu Hassan, na kwamba mimi ndiye nilikuwa kiongozi wake. Sasa nikuhakikishie kwamba mimi sio kiongozi wa Sukuma Gang, na leo hapa unana namtetea Rais Samia, nimekuthibitishia,” Gwajima alijibu.

Mbunge huyo wa Kawe aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari akimtaka Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kujiuzulu, alisema kuwa Rais Samia anafanya kazi nzuri.

“Leo siko kwenye ulimwengu wa roho, leo niko kwenye ulimwengu wa wanahabari, ninamuona kama Mama anayefanya kazi nzuri na anataka kuhujumiwa na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),” Gwajima alieleza alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari.

Juzi, Rais Samia alieleza kuwa anaona wanachama wenzake wa CCM ndio wanataka kumsumbua katika uongozi wake, akieleza kuwa wengi wana ‘msongo wa mawazo wa mwaka 2025’.

Hata hivyo, Rais Samia alisema kuwa yeye hatavunjika moyo na ataendelea kutafuta njia zote na kutumia kila fursa atakayoiona duniani kuwaletea Watanzania maendeleo kama alivyoapa.

Zoezi la uokoaji Pemba lasitishwa
Wema Sepetu ashambuliwa kisa picha ya mtoto mchanga