Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemwandikia barua rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimuomba siku tatu za kutembelea wagonjwa wa COVID 19 waliopo hospitalini ili aweze kuwaombea wapone ugonjwa huo.

”Nimemwandikia waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kassim nimemuomba anipe ruhusa maalumu mimi niende nikawaombee wagonjwa wa COVID 19, barua rasmi ndio, ikimpendeza mimi niende kule aniache pale, waone kama mimi nitakuwa na COVID 19 watu wengine nikizungumza wanaona nazungumza bra bra” amesema Gwajima.

Gwajima amesema kwa kuwa nchi yetu imeamua kukabiliana na janga hili katika milengo miwili ule wa kufuata taarifa zinazotolewa na wizara ya Afya pamoja na mlego wa kiimani hivyo ameomba apewe nafasi ili waweze kuwaombea wagonjwa wa COVID 19.

”Nimeandika barua ya unyenyekevu sana ya kumuomba muheshimiwa waziri mkuu ninaomba kama walivyo madaktari wengine kwakuwa nchi yetu imechukua milengo yote miwili, mlengo wa medicine au Wizara ya Afya na muongozo wake na Rais akatangaza maombi ya siku tatu taifa zima kuomba, haitakiwi kuishia hapo mimi nimeandika barua ya kumuomba waziri mkuu uniruhusu sasa unipe angalau siku mbili tatu nikutane na hao wagonjwa wa covid 19 tuone itakavyokuwa” ameongezea Gwajima.

Aidha Gwajima ameongezea kuwa ataenda kuwaombea watu hao na hatopata maambukizi ya virusi hivyo kama ambavyo wengi wanadhani.

Hata hivyo Serikali imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kwenda kuchukua dawa Madagascar kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo.