Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesisitiza msimamo wa kutopata chanjo ya corona iliyoingia nchini, akieleza kuwa yuko tayari hata kupoteza ubunge.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kawe alizua gumzo wiki kadhaa zilizopita baada ya kueleza kuwa chanjo ya corona haijafanyiwa utafiti wa kutosha na kwamba daktari yeyote ambaye ataitetea bila kuwa na uthibitisho wa utafiti wa kitabibu hatapona.

Akihubiri leo, Agosti 15, 2021 katika ibada ya Jumapili kanisani kwake, Ubungo jijini Dar es Salaam, Gwajima aliizungumzia tweet iliyosambaa mitandaoni ilidai ni lazima wabunge wote wapate chanjo ya corona, tweet ambayo uongozi wa Bunge uliikanusha.

“Kulikuwa na twitter inasambaa kwamba wabunge wote wachanjwe, baadaye Ofisi ya Bunge ikakanusha; nikasema hata ingekuwa kweli, mimi nisingechanjwa. Ni bora kurudi hapa nyumbani, ubunge ni mzuri una heshima unasaidia wananchi lakini kunichanja hapana,” amesema Askofu Gwajima.

Katika hatua nyingine, Gwajima amekitahadharisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) akidai kuwa si vyema wote wakapata chanjo kwani endapo itakuwa na madhara nani atapiga kampeni mwaka 2025.

“Wanaotaka nifukuzwe CCM watumie akili, kwa mfano tukichanja wote halafu kufikia 2025 watu wako hoi tunapigaje kampeni, bora wengine tubaki tusaidie kutetea chama chetu,” amesema.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye pia ni kiongozi wa dini alifafanua kuwa hapingi chanjo ya corona, lakini kinachofanya apinge ni kwa sababu anaamini chanjo hii inayotolewa haijafanyiwa utafiti wa kutosha.

Kauli ya Askofu Gwajima inakinzana na kauli na Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe ambaye alieleza kupitia kipande cha video kilichosambaa mitandaoni, akiwasihi watanzania kupata chanjo ya corona, na kwamba kuikataa kuchanjwa ni kiburi kisicho na maana.

Askofu Kakobe alisema alipata ushuhuda kutoka kwa kiongozi wa dini ambaye aliwahi kuugua corona na akapona, akieleza mateso aliyoyapata. Hivyo, aliwataka watu kutopuuzia kuchukua tahadhari, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa, pamoja na kuhakikisha wanapata chanjo ya corona.

Alihoji ni aina ngapi za vidonge na chanjo ambazo Watanzania wameshapata na kwanini wanapinga chanjo ya corona. Aliwasihi watu kutokuwa na kiburi kisicho na maana.

Polisi anayetuhumiwa kumbaka mkimbizi yamkuta mengine
Jeshi la Polisi Zanzibar yaja na mikakati kupambana na madawa ya kulevya