Aliyekuwa Msemaji wa Klabu ya Young Africans, Haji Sunday Ramadhan Manara amemuomba radhi Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohammed Mchengerwa kutokana na kauli yake ya kwamba Waziri huyo alitoa maelekezo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumpa adhabu kubwa Manara kutokana na makossa ya utovu wa nidhamu.

Manara amesema baada ya kufuatilia amegundua kuwa Waziri hakutoa maelekezo hayo kwa TFF bali ameweka viwango vya viongozi na wadau wa michezo kuheshimu mamlaka zinazosimamia michezo nchini ili kuwa na tija katika uendeshaji.

“Ndhani kulikuwa na kutokuelewa na ilichukuliwa hivyo na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao kuandika kuwa ‘Waziri amshukia Manara”, lakini na mimi niliingia kichwakichwa kwa kuwa ilikuwa wiki ileile na hata katika press conference yangu na ile ya Wazee wa Young Africans na baadhi ya viongozi wetu wa matawi ziliingia kichwakichwa kama nilivyoingia mimi.

“Sababu jambo lilitokea wiki ileile na wiki ileile na kukawa na presha ya vyombo vya habari, na mimi katika maelezo yangu nikajikosea, na nikaikosea Serikali na waziri kwa sababu nilisema waziri ametoa maelekezo kwa TFF.

“Baadaye nilipofuatilia nikazungumza na maofisa wa Wizara wakaniambia hapana, hiyo ni standard ambayo Waziri ameiweka ya kwamba lazima viongozi wa michezo waheshimu mamlaka zinazosimamia michezo, amekuwa akizungumzia suala la maadili kwa viongozi na taasisi.

“Nikagundua nia ya waziri hakulenga kujikita kwenye jambo langu bali ilikuwa ni standard ambayo ameiweka na ni jambo jema ambalo amelifanya waziri.

“Inawezekana baadhi ya watu serikalini, baraza, wizara na hata waziri mwenyewe, yawezekana hawakuelewa tafsiri ya lugha yangu niliyoisema, basi kwa utashi wa kimaadili lazima useme samahani kama kuna mmoja yeyote nimemkosea, niseme samahani,” amesema Manara.

Ikumbukwe kuwa, Manara amefungiwa na Kamati ya Maadili ya TFF kujihusisha na masuala ya soka kwa muda wa miaka miwili na faini ya Tsh milioni 20 kwa kosa la kumtolea maneno machafu na kumdharirisha Rais wa TFF, Wallace Karia.

Makamba aahidi mtambo wa gesi tani moja Peramiho
Mke wa Ne-yo ayaanika machafu ya mumewe