Mkuu wa Idara Ya Habari Na Mawasiliano ya Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC haji Sunday Manara, amekua sehemu ya wadau waliojitokeza hadharani na kujadili kwa kina suala ama pendekezo la kupunguzwa kwa wachezaji wa kigeni, kutoka kumi hadi watano, kama lilivyoibuliwa na waziri mwenye dhamana Harrison Mwakyembe siku za karibuni.

Mwakyembe anaamini idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni imekua kikwazo kwa wachezaji wazawa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye vikosi vya klabu yao, jambo ambalo linaendelea kuidhohofisha timu ya taifa (Taifa Stars).

Haji amejitokeza na kuandika makala iliyojikita kupinga mpango ama pendekezo hilo la waziri mwenye dhamana, kwa kutoa sababu ambazo anaamini bado Tanzania inahitajia kuendelea kuwatumia wachezaji wa kigeni, ambao wamekua sehemu ya chahu ya mafanikio katika soka la bongo.

Manara alianza kwa kuandika kichwa cha habari: TUNAJIANDAA KUKOSEA ZAIDI

Wakati huu janga la ugonjwa hatari wa Corona likiichachafya dunia, habari kubwa ya kispoti nchini ni kuhusiana na wazo la Mh Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini Dr Harrison Mwakyembe la kutaka kupunguzwa kwa idadi ya wachezaji wa kigeni wanaocheza katika Ligi Kuu nchini, toka kumi wa sasa na kufikia watano!!

Hoja ya Waziri ni kuwa wachezaji wa kigeni wanawanyima wachezaji wetu wazawa fursa zaidi ya kucheza na hatimae kutokuwa na kikosi bora cha Timu ya Taifa.

Hapa ndio tunapojiandaa kukosea zaidi, maana huko nyuma tushakosea sana kiasi cha kwamba leo Tanzania sio nchi bora katika mchezo huo unaopendwa zaidi duniani, tumekosea kwenye mipango yetu na maamuzi yetu kama hayo, lakini tunaona haitoshi na sasa tunajiandaa kukosea zaidi ili Tanzania isifanikiwe kisoka.

Ndio makosa yetu ni kuona Tanzania ni kisiwa na inaweza kuja na mikakati na mipango tofauti na tukaweza kuwa Bingwa wa Afrika na hata dunia.

Tunaweza kufuta mashindano ya vijana na watoto kote kuanzia ngazi za mtaani hadi mashuleni na tukawa na ligi bora duniani…

Tunaweza kuviachia viwanja vya watoto kuwa makontena ya kuuzia pombe na bado tukawa na rundo la vikombe vya kimataifa, tunaweza kugeuza viwanja vya Jangwani stand ya mabasi Na bado siku moja Tanzania ikamtoa Messi na Ronaldo kwa wakati mmoja, kiufupi Tanzania tunajua kuliko Misri au Ghana katika soka na tuna mipango mizuri kuliko hata Uholanzi , labda tunawazidi kidogo tu Morocco na Brazil!!!!

Wakati nchi nyingi zinategemea uzalishaji wa wachezaji wadogo ktk vituo vyake imara vya mafunzo ili kuwa na timu bora ya taifa, siye tunafikiria kuwa na ligi ya wazawa watupu kina Makumbi Juma na Moses Mkandawile!!

Wakati nchi nyingine za kiafrika zinajitahidi kuwawekea mazingira rafiki na kutoa fursa zaidi kwa wachezaji wao kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya ili wawe na kikosi bora cha timu ya taifa, sie tunaona dawa ya timu imara ya taifa ya Tanzania ni kuwapunguza kina Kagere na Morrison na kuwaachia kina Tenende na Kayeta wawe peke yao ili tupate Taifa Stars ya ahadi!!

Sijui tunafeli wapi??

Tunaendelea kuchagua kushindwa kila siku kwa mipango ya kivyetu kivyetu, kwa mikakati ya “Kisiwa'” chetu chenye wajuzi kuliko nchi yoyote Ulimwenguni, kisiwa ambacho sio ajabu kukuta Mwanasiasa anageuka kocha wa mpira na daktari wa binadaam kuwa Mkurugenzi wa idara ya michezo nchini.

Wakati nchi nyingi kama sio zote Afrika zinatumia wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya bara hili kwenye timu zao za taifa, kisiwa chetu cha wajuzi kinafikiria kiendelee kuwatumia kina Ikupilika Nkoba wa Lipuli kuwafunga kina MO Salah wa Liverpool na Misri na kina Mahrez wa Manchester City na Algeria, hii ni kuamua kushindwa Asubuhi tu!!

Hivi hatujui kuwa bila wale wachezaji wa nje ya nchi Simba isingeweza kufuzu Kwenye hatua ya makundi na hatimae robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika??

Labda tuna lingine, lakini kwa hili la kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni katika ligi kuu halitusaidii timu ya taifa wala mpira wetu kwa ujumla!!

Zama zimebadilika na mpira wa miguu umebadilika sana, Soka sasa ni biashara kubwa duniani, Soka sasa sio mchezo wa wanasiasa kutengeneza majina yao ni mchezo wenye weledi na unaingiza mapato makubwa kuliko mchezo wowote kote Ulimwenguni na Tanzania ikiwemo!!

Sizungumzii mapato ya milangoni pekee, fikiria kodi ambayo Serikali yetu inapata kutokana na sekta hii iliyojirasimisha yenyewe, fikiria pia uwanja ule mkuu wa taifa ungepataje idadi ya mashabiki elfu sitini bila shughuli za uhakika za kina Kagere na Cleotus Chama?

Hebu ngoja niulize kabla ya ujio wa hao wachezaji kumi wa kigeni lini tushawahi kucheza kombe la dunia? Lini tushawahi kuwa Mabingwa wa Afrika?

Wakati wanacheza kina Kiwelo Mussa na Ibrahim Magongo pamoja na waswahili pekee yao tushawahi kufuzu hata mashindano ya vijana chini ya miaka kumi na saba ktk ngazi ya dunia?

Halafu tupige hesabu nyepesi tu, Vilabu vya Ligi kuu vipo ishirini, ni klabu tatu pekee zenye idadi ya wachezaji kumi kumi wasio raia Tanzania, kwa hiyo ni wachezaji thelathini tu labda na ziada nyingine kumi toka katika vilabu vingine kati ya wachezaji zaidi ya mia tano wanacheza Ligi kuu, sasa hao wachezaji Arobaini ndio wanaofanya tusifanye vizuri timu ya taifa??

Hao wengine wanashindwa nini kutupeleka World cup?

Waingereza walianzisha utaratibu huu na ikaja kuwagharimu baada ya kuona vilabu na hata timu yao ya taifa haikufaidika na “ubaguzi” huu usio na tija!!

Serious unaweza kumfunga Mazembe na kina Boko peke yao bila uzoefu wa kina Morrison na Chirwa?

Nisiandike maneno mengi nikamkwaza Waziri wangu na Baba yangu, ambae aliwahi kuniambia Baba yako Sunday ni zaidi ya Okocha uwanjani, ila kwa hili Daktari Bingwa wa Sheria itakuwa Kwa bahati mbaya hukulitafiti (kama PhD inavyotaka).

Serikali ije na mpango wa uwekezaji ktk uwanda wetu huu wa Soka, ije na mpango wa kusomesha watu wetu wawe makocha bora.

Isomeshe wataalam wetu wa mambo ya utawala katika michezo, itujengee Football Academies za kisawasawa kama za nchi za wenzetu, halaf tuone kama Simba, Azam na Yanga watahangaika kuwasaka kina Molinga na Yakubu, tukizalisha Wachezaji wa uhakika toka kwetu, kwa nn tumtafute Cleutus Chama??

Kwa nini Azam FC wawe na kipa mwenye mikono mia kama Abarloa??

Mbona Simba inae Jonas Mkude na haihangaiki kusaka mbadala wake?

Cha ajabu Simba na Azam FC ndio timu zenye vikosi imara vya vijana na asilimia kubwa ya wachezaji wanaocheza katika vilabu vingi vya ligi kuu wamezalishwa pale.

Wao na Yanga wanafikiria kushindana na Wakubwa wenzao huko, unafikiria kumfunga Esperence na Masatu Magesa??

Ahhh Mzee wangu Mwakyembe, tuonee huruma kidogo, tutashindwa kutimiza ahadi ya Mh Rais kuleta kikombe cha Afrika, tutakuwa kama miaka ile, raundi ya awali tu OUT!!

Haji S. Manara.

27/04/2020

Said Ndemla: Hakuna nilichoposti wala kuongea
Kim Jong-un azungumza kwa mara ya kwanza tangu azushiwe kufa