Msemaji wa klabu ya Young Africans Haji Sunady Ramadhan Manara ameweka nadhiri ya kuhama nchi, endapo klabu hiyo itashindwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22.

Manara ameweka nadhiri hiyo akiwa kwenye kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM leo Alhamis (Januari 27), ambapo amesema hakuna la kuwazuia kufanya hivyo, baada ya kusubiri kwa miaka minne.

Amesema Young Africans ina kikosi cha kutimiza dhamira ya kutwaa ubingwa msimu huu na hana shaka na hilo, ndio maana ameweka nadhiri hiyo hadharani.

“Tukikosa ubingwa msimu huu mimi nitahama nchi, nitachana passport yangu na kila kitu, yaani Yanga hii ikose ubingwa? tufungwe michezo minne sisi ili tupoteze sifa hii ya kuwa mabingwa wa msimu huu? Haiwezekani!”

“Huwa ninafurahishwa sana na vichekesho vinavyoendelea huko, kuna watu wanasema Yanga imekua kawaida yao kuongoza halafu sisi tunakuja kuchukua ubingwa, hivi ni vichekesho jamani, watu wanaishi kwa mazoea, yaani kwa Yanga hii usubiri hilo litokee, kweli mimi nitahama nchi.” amesema Manara.

Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 35, baada ya kucheza michezo 13, ikiwaacha Simba SC kwa tofauti ya alama 10.

Ed Sheeran aishi miaka 7 bila kutumia simu ya mkononi
Watoto wenye matatizo ya moyo wapata ahueni JKCI