Serikali Rwanda  imetangaza katazo la kuingia ama kutoka katika mji mkuu wa nchi hiyo Kigali, kutokana na hali ya kutisha ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Kulingana na kikao cha Baraza la Mawaziri hatua ya kupiga marufuku usafiri wa umma na kibinafsi kati ya wilaya na mji mkuu Kigali inaanza kutekelezwa leo.

Serikali ya nchi hiyo imesema hali imekuwa mbaya na ya kutisha kutokana na kuongezeka sana kwa visa vya maambukizi pamoja na vifo vya watu  ambapo  katika kipindi cha wiki moja tu Rwanda imerekodi watu 30 waliokufa kutokana na ugonjwa huo.

Takwimu zinazotolewa na maafisa wa afya wa Rwanda zinaonyesha kwamba jumla ya watu 105 wameshafariki dunia kutokana na Covid 19 ambapo nusu yao walipoteza maisha mnamo Desemba tu.

Akizungumza na Radio ya taifa ,Daktari Tharcisse Mpunga anayesimamia huduma ya msingi ya afya ameeleza kwamba “katika kiwango hiki nchi inapaswa kutekeleza sheria ya kutotoka nyumbani kote nchini ” lakini ‘‘hatukupenda maisha yasimame kabisa’’.

Katika hatua mpya zilizotangazwa jana usiku wa manane , biashara zote ziliamriwa kufungwa saa kumi na mbili jioni , mikusanyiko yote ya kijamii na hafla imepigwa  marufuku, na amri ya kutotoka nje kuanzia saa mbili usiku hadi saa kumi alfajiri imebaki.

Aidha, imetangazwa kwamba watalii wa ndani na wa kimataifa wanaweza kusafiri kote nchini lakini baada ya kupima covid 19 na kuthibitisha kuwa hawana maambukizi ya ugonjwa huo.

Katika siku saba zilizopita Rwanda imerekodi idadi isiyo ya kawaida ya visa 820 na vifo 30 huku Maafisa wa Afya wa Rwanda wakiamini kuwa ongezeko la maambukizi huenda lilichangiwa na sikukuu za Krismasi na mwaka mpya ambapo watu walisafiri sana kwenda maeneo yao asilia .

Athari za hatua mpya tayari zimeanza kujitokeza ikiwa watu waliosafiri kwenda katika maeneo yao asilia kwa ajili ya sikukuu wamekosa jinsi ya kurejea mjini Kigali ili kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Benchi la ufundi Gwambina FC lapigwa chini
TCRA yaifungia Wasafi TV