Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewaagiza Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kuendelea na kazi katika maeneo yao kwa siku zote zikiwemo sikukuu.
 
Ametoa maagizo hayo akiwa Kongwa jijini Dodoma alipokuwa akikagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini ambapo pia aliwasha umeme katika vijiji vya Ngonga na Mjini Mashariki B.
 
“Wakandarasi, najua kuna sikukuu lakini hakuna sikukuu kwenye kazi za umeme. Jipangeni na magenge yenu, Mameneja na vibarua muendelee na kazi. Hakuna Pasaka kwenye umeme. Umeme ni usalama na umeme ni uhai,” amesema Dkt. Kalemani
 
Aidha, Waziri pia amemwagiza Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Kongwa, kuwaunganishia umeme wananchi wa kijiji cha Ngonga ambao nyumba zao zimerukwa.
 
Akihamasisha kuhusu matumizi ya UMETA, Waziri Kalemani amewataka viongozi mbalimbali wa Halmashauri za Vijiji na Wilaya kuhakikisha wanatumia kifaa hicho katika Taasisi za Umma ambazo majengo yake hayana vyumba vingi ili kupunguza gharama za kutandaza nyaya za umeme.
 
Katika ziara hiyo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, ambaye ndiye Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai, alitoa salamu za shukrani kwa serikali kwa kuwapelekea wananchi wake umeme kwa ajili ya maendeleo yao.

8,004 wafariki, 35,231 wajeruhiwa kwa ajali za bodaboda
Baada ya kipigo, Manara amvaa Zahera, 'Unatakiwa ujifunze kuongea mnapofungwa'