Mbunge wa jimbo la Kawe, Halima Mdee amezungumzia uamuzi wa Rais John Magufuli kuweka hadharani mshahara wake akijibu hoja za wanasiasa wa vyama vya upinzani nchini.

April Mosi, Rais Magufuli alitumia kipindi cha Clouds360 cha Clouds TV kueleza kuwa mshahara wake ni shilingi milioni tisa na laki tano (9,500,000), kiasi ambacho kinazidiwa na mishahara ya watumishi wengi nchini.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika jimbo la Mtama mkoani Lindi, Mdee alimtaka Rais Magufuli kuweka wazi pia posho anazopata ili zifahamike kwa wananchi wote kama ilivyo kwa posho na mishahara ya wabunge.

“Juzi Rais anasema eti mshahara wake Sh9.5 milioni, sasa atutajie posho za kila siku ili kila Mtanzania ajue kiasi ambacho anakipata. Sisi wabunge mshahara wetu katika hati ya mshahara unasomeka Sh3 milioni, lakini posho na pesa ya mambo ya utendaji ya mbunge inafika Sh10 milioni, Rais atuambie na yeye posho zake ni kiasi gani,”,” alisema Mdee.

Awali, Mbunge wa Kigoma Mjini alimtaka Rais Magufuli kutangaza mshahara wake ikiwa ni miaka michache tangu akaririwe akidai kuwa Rais wa awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete alikuwa analipwa zaidi ya shilingi milioni 30, taarifa zilizokanushwa na ikulu licha ya kutotoa takwimu husika.

PSG Wajipanga Kuvunja Rekodi Ya Usajili Duniani
Memphis Depay Atumika Kuvujisha Siri Za Man Utd