Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri 100 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 100 au zaidi ya lengo la mwaka.

Bashungwa ameyasema hayo hii leo Agosti 2 , 2022 Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa kuhusu Mapato na matumizi ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Amesema, Halmashauri 78 zimekusanya kati ya asilimia 80 hadi asilimia 99, na Halmashauri 7 zimekusanya kati ya asilimia 58 hadi 79 na kwamba zilizofikia malengo ya mwaka zimeongezeka kutoka Halmashauri 57 katika mwaka wa fedha 2020/21, hadi kufikia Halmashauri 100 katika mwaka wa fedha 2021/22.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa, akitoa taarifa kuhusu Mapato na matumizi ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka wa Fedha 2021/2022, hii leo Agosti 2, 2022 jijini Dar es Salaam.

“Ulinganisho wa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, kwa kigezo cha asilimia ya makusanyo, unaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imeongoza katika Halmashauri zote kwa kukusanya asilimia 247 ya makisio yake ya mwaka.

Bashungwa ameongeza kuwa, Halmashauri zilizofuata ni za Wilaya ya Mlele asilimia 185, na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro asilimia 158 huku Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli ikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 58 ya makisio yake ya mwaka.

“Halmashauri ya Bumbuli inafuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe iliyokusanya asilimia 67, na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda asilimia 70 ya makisio yake ya mwaka na katika kuzipima Halmashauri zote kwa Kigezo cha wingi wa mapato, jumla ya Halmashauri 35 zimekusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 5,” amefafanua Waziri Bashungwa.

Kuhusu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Waziri amesema imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote, kwa kupata Shilingi Bilioni 75.3 ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Shilingi Bilioni 47.3, na Halmashauri ya jiji la Dodoma Shilingi Bilioni 45.1.

Hata hivyo, Bashungwa amebainisha kuwa jumla ya Halmashauri nne zimekusanya chini ya Shilingi Bilioni 1, huku Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli ikiwa ya mwisho kwa kukusanya Shilingi Milioni 599.7, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Shilingi Milioni 692.1, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Shilingi Milioni 792.3, na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Shilingi Milioni 880.2.

Mabadiliko makamanda wa Polisi
Mandonga amuibukia Rais wa Young Africans