Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kutoka Mikoa ya Arusha na Geita wamewapongeza viongozi Mkoani Simiyu kwa ubunifu waliofanya kuanzisha kambi za kitaaluma kwa ajili ya kuongeza ufaulu na kutoa wito kwa viongozi wengine kuiga ubunifu huu ili waweze kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa NEC (Arusha) Anna Agatha Msuya na Idd Kassim Idd Mjumbe wa NEC(Geita) mara baada ya kutembelea wanafunzi wa Kidato cha Sita mwaka 2019 walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, mara baada ya viongozi hao kuungana na Mjumbe wa NEC kutoka Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Gungu Silanga kukabidhi msaada wa chakula kwa wanafunzi hao.

Agatha Msuya amesema kuwa laiti kambi hizo zingekuwa zinafanyika katika maeneo mengi matokeo ya Mitihani hususani ya Taifa yangekuwa mazuri zaidi ya sasa kwani zimeonekana kuusaidia mkoa wa Simiyu kupanda kielimu.

“Nimevutiwa na ubunifu wa Simiyu kuwa na kambi za kitaaluma, tungekuwa na matokeo mazuri kama tungekuwa na viongozi wa Serikali wabunifu kama hapa Simiyu, naomba tulichokiona Simiyu kifanyike na mikoa mingine, mwaka juzi walikuwa wa 26 Kitaifa, mwaka jana wakawa wa 10 na naamini kwa kambi hii hatutaikosa Simiyu katika mikoa mitano bora,”amesema Msuya.

Kwa upande wake, Idd Kassim Idd Mjumbe wa NEC(Geita) pamoja na kupongeza juhudi za mkoa wa Simiyu katika elimu, ameahidi kuwa amejifunza kupitia kambi hiyo ya kitaaluma na kulichukua wazo hilo kwajili ya kushauri viongozi wa mkoa wa Geita kuona namna ya kulifanyia kazi ili kuwa na ufaulu mzuri.

Naye Mwl. Ezekiel Mollel mwekezaji katika Sekta ya Elimu amesema kuwa suala la kambi za kitaaluma ni la kipekee kwa mkoa wa Simiyu, hivyo akatoa wito kwa mikoa mingine kuiga huku akiwaomba wadau mbalimbali wa elimu kuendelea kuchangia mahitaji mbalimbali ya wanafunzi walio katika kambi ili waweze kujifunza kwa amani wakiwa na mahitaji ya msingi.

Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzao wa kidato cha Sita mwaka 2019 walioko kambini, Hidaya Simba (Maswa Girls) na Masanja Ng’hwenu (Meatu) wamewashukuru viongozi hao kwa msaada wa chakula walioutoa na kuahidi kuwa shukrani yao kubwa kwa walimu, viongozi, wazazi na wadau wa elimu wanaowasaidia ni kufanya vizuri na kuifanya Simiyu iwe nambari moja.

Pamoja na kilo 1000 za mchele na kilo 400 za maharage  zilizotolewa na Mjumbe wa NEC (Simiyu), Emmanuel Gungu Silanga, Idd Kassim Idd Mjumbe wa NEC(Geita) ametoa kilo 200 za mchele, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Simiyu ametoa kilo 100, Mdau wa Elimu Ezekiel Mollel kilo 50 na Anna Agatha Msuya Mjumbe wa NEC (Arusha) ameahidi kutoa zawadi kwa wanafunzi watakaopata daraja la kwanza(divion one)

TANAPA yachangia ujenzi wa Zahanati mkoani Kagera
Dkt. Yonaz akabidhi Kompyuta mkoani Simiyu