Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amezionya Halmashauri zote mkoani Rukwa kuhakikisha wanazitumia vizuri Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD) kwa kuongeza mapato katika halmashauri zao.

Zelote amesema hayo katika kikao maalum cha kujibu hoja za ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa madiwani wa  Manispaa ya Sumbawanga katika kumalizia ziara yake maalum kwa Halmashauri zote mkoani humo kujua namna Halmashauri zilivyojipanga ili hoja hizo zisijirudie miaka inayofuata.

“Katika kila sehemu za mauzo lazima mashine hizi ziwepo na kuwepo sio mtindo huu (akionyesha msururu wa risiti zilizokatwa tayari kwa matumizi) hizi nimezikamata maeneo anajua Mkurugenzi, asubuhi watu wanagawana, ndio mchezo uliopo, pamoja na jitihada tunazofanya bado watu wanatafuta mbinu za kuiba, hii sio kwamba nimeleta iwe mfano, hapana, nimezikamata na mfahamu kuwa mimi ni mtaalamu wa kukamata,” Amesema Zelote

Pia amesisitiza suala la uwazi wa matumizi ya fedha za halmashauri kwa waheshimiwa madiwani, ambapo ametaja majukumu kadhaa ya Mkurugenzi wa Halmashauri na kusema kuwa moja ya kazi za Mkurugenzi ni kuhakikisha kuwa madiwani wanapata taarifa za fedha za halmashauri.

“Hapa mmezungumza na mmenionyesha kwa kiasi kikubwa kwamba hamnazo taarifa na nikiangalia kazi moja wapo ya waheshimkwa madiwani ni kiusimamia matumizi ya fedha za halmashauri zao sasa mtasimamiaje ikiwa hamna taarifa,” Amesema.

Katika kikao hicho mkuu wa mkoa huyo pia alimtambulisha mtaalamu wa TEHAMA ili awaelezee waheshimiwa madiwani namna mifumo ya fedha inavyofanya kazi ili nao wawe na uelewa mpana katika kufuatilia mapato na matumizi ya halmashauri.

“Suala la kukusanya mapato limekuwa likiimbwa asubuhi, mchana na usiku, kuwa tuhakikishe tunajipanga vyema kukusanya mapato ya halmashauri kwa kupitia utaratibu uliopo, suala la kutumia hizi mashine sio la kuhoji tena mwisho ulikuwa mwezi wa tatu ndio agizo lililopo kwa wakurugenzi kuwa mashine hizi ziwepo na zinafanya kazi,” Amesema

 

PPF yawakumbuka wananchi wa Mafinga
Marekani yakanusha kuwa na uadui na Korea Kaskazini