Halmashauri ya Mji wa Njombe imepokea ugeni wa Madiwani wakiambatana na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga lengo ikiwa ni kujifunza na kuongeza maarifa kuhusiana na masuala ya mapato na usafi wa Mazingira.

Hayo yamebainishwa wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha wageni hao ambapo ugeni huo umekiri wazi kuwa wamevutiwa kufika katika Halmashauri ya Mji wa Njombe kujifunza kutokana na sifa ambazo Halmashauri imekuwa ikijizolea kila mara katika eneo la usafi wa Mazingira pamoja na ukusanyaji mapato.

“Halmashauri ya Mji Sumbawanga kwa mwaka wa fedha 2017/2018 tulikasimia kukusanya bilioni mbili na milioni mia tano, lakini hatukufanikiwa kukusanya asilimia 80 kwa mujibu wa maagizo ya Waziri Mkuu, tulikusanya asilimia 54 pekee, kwa upande wa mashindano ya usafi na Mazingira tulishika nafasi ya pili kutoka mwisho kutokana na ukosefu wa vyoo bora na matumizi bora ya vyoo.”amesema Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justin Emmanuel Malisawa.

Aidha, amesema kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili ni kwenye utekelezaji wa sheria ndogo ndogo za Halmashauri na changamoto kutoka kwa wanasiasa ambao wamekuwa wakipinga na kutotekeleza ipasavyo baadhi ya maazimio waliyojiwekea kwenye ukusanyaji wa mapato na utunzaji Mazingira na ndio maana waliona umuhimu wa kuja kujifunza kutoka Njombe.

Kwa upande wake Afisa Mazingira Halmashauri ya Mji Njombe, Lawi Bernard amesema kuwa licha ya kuwa na mwamko chanya wa wananchi kwenye uchangiaji wa tozo za taka, Halmashauri kupitia mapato ya ndani imekua ikiona umuhimu wa kuiwezesha idara hiyo na ndio maana kwa mwaka wa fedha 2018/2019 walifanikiwa kutenga fedha kupitia mapato ya ndani na kununua trekta kwa ajili ya kubeba taka na hivyo kuzuia mlundikano wa taka katika maeneo ya Mji kutokana na uwepo wa vitendea kazi vya kutosha.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe, Edwin Mwanzinga amesema kuwa, siri ya mafanikio ni umoja baina ya Waheshimiwa Madiwani na wataalamu kwani wamekuwa wakipokea maelekezo ya wataalamu na panapokuwa na mapungufu wamekuwa wakishirikiana kuboresha kwa manufaa ya Halmashauri nzima.

Hata hivyo, Madiwani na Wataalamu kutoka Manispaa ya Sumbawanga wameishukuru Halmashauri ya Mji Njombe kwa elimu waliyoipata na wamepongeza ujenzi wa kiwango cha hali ya juu unaoendelea katika kituo kipya cha Mabasi na wameahidi kutengeneza mtandao wa mawasiliano na Halmashauri ya Mji Njombe ili kuendelea kupata ujuzi na mbinu mpya katika maeneo mbalimbali.

Shil. Mil. 3 zamsweka ndani mwenyekiti wa AMCOS
Video: Taasisi ya Tanzanite kuipaisha Tanzania kimataifa

Comments

comments