Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML, imesaini Mkataba wa Makubaliano na Halmashauri ya Mji Geita, Wilaya ya Geita pamoja na Halmashauri za Wilaya za Chato, Bukombe na Mbogwe kutekeleza Mpango wa Uwajibikaji wake kwa Jamii – CSR, kwa mwaka 2022/2023 wenye thamani ya Shilingi 19 bilioni.

Makubaliano hayo yametiwa saini Machi 21, 2023 mjini Geita na kushuhudiwa na Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela, wakuu wa wilaya za mkoa huo na wadau wengine ambapo jumla ya Sh. 9.8 bilioni zimetengwa kwa ajili ya Geita mji na Wilaya ya Geita, bajeti ya Shilingi 8.6 bilioni imetengwa na GGML pia itatoa milioni 600 za miradi ya maendeleo kwa Halmashauri tatu za Mbogwe, Chato na Bukombe mkoani Geita ambapo kila moja itapata shilingi milioni 200.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Geita Gold Mining Limited, Elder Damon amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni jambo muhimu na linathibitisha dhamira njema ya kampuni hiyo kwa jamii iliyowakaribisha, Serikali ya Tanzania na watu wake kwa kufuata matakwa ya Sheria ya Madini ambayo yanazingatia Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii.

Mwanasheria Mkuu wa GGML, David Nzaligo (kulia) akisaini makubaliano hayo kwa niaba ya kampuni hiyo huku upande wa Halmashauri ya Mji Geita ukisainiwa na Mwanasheria wake na chini ya  Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Zahara Michuzi.

Amesema mpango wa CSR wa mwaka huu ni mwendelezo wa mipango ya awali unaolenga kujumuisha maendeleo yaliyofikiwa na GGML hadi sasa katika maeneo ya mazingira, miundombinu, afya, elimu na biashara ndogondogo na za kati (SMEs) katika jamii ya mwenyeji wa Geita.

“Binafsi inanipa furaha kubwa kushuhudia matokeo ya miradi yenye mafanikio katika maisha ya Watanzania, hasa wale wanaoishi karibu na mgodi. GGML inajitahidi kuunga mkono matarajio ya Serikali ya Tanzania ya maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika jamii zinazowapokea.”

Aidha, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema watu wengi hawafahamu kwamba kabla ya sheria ya madini ya mwaka 2010 kufanyiwa marekebisjo mwaka 2017, tayari GGML ilikuwa inatekeleza mpango wa CSR kwa kutoa zaidi ya Sh bilioni 9 kugharamia miradi mbalimbali ya kijamii mkoani Geita.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Geita Gold Mining Limited, Elder Damon pamoja (kulia) na wawakilishi wa wilaya ya Bukombe wakionesha mikataba ya makubaliano waliyosaini leo Jumanne mjini Geita kutekelezaji wa mpango wa huduma kwa jamii (CSR) wa GGML. Bukombe pia imepata Sh 200 kati ya Sh bilioni 19 zilizotolewa kwa wilaya za mkoa huo.

“Hata baada ya kuingiza kipengele hicho cha uwajibikaji wa kampuni kwa jamii -CSR, sisi tulikuwa wa kwanza kufanya hivyo kwani kila mwaka tunatumia walau Sh bilioni 9.2 hadi 10,” alisema Simon Shayo. Kipindi cha mwaka 2015 hadi 2017 tuliona ni muhimu kuongeza kwa kiasi kikubwa fedha tunazowekeza kwenye jamii ili kutengeneza uchumi mbadala hata mgodi ukifungwa,” alisema Shayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, alisema ni furaha kushuhudia tukio hilo likifanyika kipindi ambacho wanaadhimisha miaka miwili tangu Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Dkt. Samia Suluh Hassan kuanza kazi ya kuongoza taifa maendeleo yake ikiwemo ya sekta ya madini.

Aidha, alitoa wito kwa wana-Geita kuchangamkia fursa za miradi hiyo kwa kuhakikisha mahitaji ya wakandarasi yanapatikana ndani ya mkoa huo na kuagiza Viongozi wa halmashauri kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi ili kutoacha mapungufu yoyote.

Shambulio lauwa 41, idadi kubwa Wanawake, Watoto
Viongozi pambaneni ukatili wa kijinsia, watoto: Dkt. Gwajima