Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatoa asilimia 10% ya mapato yake kwa Wanawake, Vijana na Walemavu kwa mujibu wa sheria.

Ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi katika Viwanja vya TASAF wilaya ya Sikonge mkoani Tabora ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo.

Amezitaka halmashauri kuweka utaratibu mzuri kuhakikisha fedha zinazokopeshwa kwa vikundi zinarejeshwa kwa kuwa lengo la fedha hizo ni kuwanufaisha walengwa zaidi huku akishauri kuwepo na makundi yenye mradi unaoleta tija kwa manufaa ya wengi.

Niagize Halmashauri zote kuhakikisha zinatoa fedha hizo kama ilivyopangwa bila riba yeyote kwani fedha hizi zipo kisheria na kwa kutozitoa ni kuvunja sheria”amesema Makamu wa Rais.

Aidha, katika hatua nyingine Makamu wa rais ametoa wito kwa wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kutoharibu mazingira kwa kukata miti kwani hasara ya kukata mti ni kubwa kulikoni faida wanayoipata hivyo amewashauri kutumia teknolojia mpya ya Solar na Umeme kama ilivyoshauriwa na wataalamu.

Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Sikonge ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amesema kuwa mpaka 2021 kwa mara ya kwanza vijiji vyote wilayani Sikonge vitapata umeme wa uhakika.

Naye Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kurudisha uchumi wa madini kwa Watanzania.

Katika ziara hiyo Makamu wa Rais ameongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba, Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri Maji, Juma Aweso, Naibu Waziri Ujenzi, Elias Kwandikwa, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Angelline Mabula na Naibu Waziri TAMISEMI,  Mwita Waitara

Kauli zamponza Halima Mdee, adondokea mikononi mwa Polisi
Majaliwa amkaanga Mkurugenzi wilaya ya Rombo, 'Nakupa siku 16'