Taarifa hii ni kwa hisani ya shirika la habari la BBC Swahili

Wiki saba baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, Hamid Mir alisimama mbele ya mtu aliyetuhumiwa kupanga na kutekeleza mashambulizi hayo kutoka maeneo yasiyojulikana mjini Kabul. Yalikuwa mahojiano ya mwisho aliyofanya na Osama bin Laden.

Mahojiano hayo yalifanyika katikati mwa mashambulio mengine dhidi ya Marekani. Lakini hii haikuwa mkutano wa kwanza kati ya mwandishi huyo maarufu wa Pakistan na kiongozi huyo wa al Qaeda.

Mara ya kwanza Mir alikutana na Bin Laden, hakujua mengi kumhusu. Baada ya mkutano wa pili aligundua kuwa ni mtu “hatari sana.” Wakati alipomhoji mara ya tatu dunia ilikuwa imebadilika kabisa.

Alipoulizwa kama aliogopa kufanya mahojiano hayo alisema kuwa aliogopa mashambulio ya mabomu zaidi kuliko kiongozi huyo wa al Qaeda.

Línea

Uliwezaje kuwasiliana na Osama bin Laden?

Ni hadithi ndefu. Mwaka 1997 niliandika nakala iliyoangazia jinsi Marekani ilivyosaidia Taliban na kwamba inaishinikiza serikali ya Pakistan kuwaunga mkono, na walitaka kuwatumia kutoa ulinzi kwa kampuni ya mafuta ya Marekani, Unocal.

Nakala yangu ilipochapishwa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan wakati huo, Benazir Bhutto, alinipigia simu kujaribu kuelezea msimamo wake, akisema haungi mkono itikazi ya Taliban lakini aliwasaidia tu kwa sababu za kimkakati.

Pia aliongeza kuwa serikali yake hakuwa na uhusiano wa kirafiki nchini Afghanistan bali ilikuwa inalinda bomba la mafuta la Turkmenistan-Pakistan.

Alinielekeza kwa waziri wake wa mambo ya ndani, Jeneral Naseerullah Khan Babar, ambaye alirudia yale yaliyosemwa na Waziri Mkuu.

Alijitolea kunisaidia nikutane na baadhi ya viongozi wa Taliban huko Kandahar (Afghanistan) na hatimaye nikaenda kukutana nao.

Walighadhabishwa na taarifa yangu.

Waliniambia kwamba Radio ya Iran inamnukuu Hamid Mir, ambaye aliandika taarifa inayodai Taliban wanafanyia kazi Wamarekani.

Kisha wakaniuliza: “Je! Unajua kwamba tunamhifadhi adui mkubwa wa Marekani?

Nikasema sijui ni nani. “Osama bin Laden”, walinijibu.

Wakati huo sikumjua

Ushawahi kumsikia?

La, Sikujua lolote kumhusu. Na wakati huo nikaandika jina lake kwa mara ya kwanza.

Waliniambia wanaweza kupanga mkutano kati yangu na Osama, kwa masharti kwamba baada ya hapo nisiandike kuwa wanawafanyia kazi Wamarekani. Nilisema, “Sawa, hakuna shida.”

Ilikuwa vigumu kumpata?

Haikuwa vigumu kumpata kwa sababu hakukua na vikwazo mpakani. Ilikua mwaka 1997.

Tulienda Jalalabad ,ambayo iko upande wa mashariki wa Afghanistan,kutoka hapo tukapitia milima maarufu ya Tora Bora hadi hadi kwenye makao makubwa ya pangoni, na hapo kulikuwa na kiongozi maarufu wa Taliban, Maulvi Younis Khalis, ambaye alinikaribisha.

Baada ya hapo tulipitia mchakato mgumu wa kiusalama, kupekuliwa mwili. Walinzi wanapekua hadi chini ya mabazi yako ya ndani nilikwazika sana kusema kweli.

Baada ya hapo nilikutana na Osama bin Laden, ambaye aliomba radhi kwa niaba yao.

“Pole sana ,” alisema, “lakini huo ndio mchakato wa usalama. Wanamfanyia hivyo kila mtu, hata jamaa wa familia yangu.”

Kwa hivyo mkutano wetu wa kwanza ulianza kwa neno “samahani.”

Bin Laden alikuwaje wakati huo? Muonekano wake kwa jumla?

Kusema kweli , hakuwa mtu maarufu na mimi sikujua mengi kumhusu.

Mlizungumza kuhusu nini?

Kwanza kabisa wakati huo, mwaka 1997, katika mahojiano yangu ya kwanza, alikuwaa napendekeza muungano wa Taliban na Iran na China.

Taliban haikuwahi kuwa na uhusiano mzuri na Iran, kwa hivyo nishangaa kwa nini mtu huyu anapendekeza muungano waTaliban na China na Iran.

Kitu cha pili alichosema ni kwamba Marekani haitaendelea tena kuwa nchi yenye uwezo mkubwa dunini. Hii ilikuwa mwaka 1997.

Alipotoa madai hayo kabla ya shambulio la 9/11.

Mahojiano ya pili yalifanyika wapi?

Yalifanyika Kandahar mwaka 1998, wakati alipotoa muelekezo ( fatwa )kuhusu mauaji ya Wamarekani.

Mahojiano hayo yaliangazia zaidi itikadi yake. Yalikuwa mazungumzo marefu, pengine kama saa nne au tano.

Mahojiano ya kwanza ya Hamid Mir na Osama bin Laden.
Maelezo ya picha,Mahojiano ya kwanza ya Hamid Mir na Osama bin Laden.

Niliikabili. Nilihoji kwamba itikadi yake ilikwenda kinyume na kanuni za msingi za Uislamu kwa sababu, kulingana na mafundisho ya Kiislamu, damu ya mtu asiye Muislamu asiye na hatia ni sawa na damu ya Muislamu.

Alimwambia ikiwa anataka kuua wasio Waislamu ambao hawana hatia, huo haukuwa Uislamu.

Alikuwa anajaribu kuhalalisha itikadi yake juu ya mauaji ya Wamarekani.

Alisema kuwa raia wa kawaida wa Marekani hulipa ushuru kwa serikali yao, wanapigia kura serikali yao, wanachague serikali yao. Kwa hivyo wanaunda sera za kupinga Waislamu.

Ndio sababu alihalalisha kuua Wamarekani wote. Ilikuwa ni hoja dhaifu sana.

Je ulijua kwamba alichosema kitakuja kutokea?

Mahojiano hayo yalifanywa Mei mwaka 1998 na siku chache baadaye kulitokea masambulizi ya mabomu dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania.

Al Qaeda haikuwahi kukubali kuhusika na mashambulio hayo, lakini ilishukiwa kuyatekeleza.

Baada ya mahojiano ya pili niligundua kweli kwamba alikuwa mtu hatari sana. Alikuwa gaidi maarufu na mtu anayetafutwa sana baada ya mahojiano hayo.

Baada ya Septemba 11, 2001 ulitafutwa tena mara ya tatu kukutana na Bin Laden. Je mara hiyo ilikuwa tofauti?

Ilifanyika wiki saba baada ya mashambulio hayo. Nililala siku moja Jalalabad, siku mbili mjini Kabul. Hata watu wake hawakujua mahali alipokuwa.

Kwa hivyo tulikua tukimsubiri mjini Kabul. Lakini huenda hakuwa hako. Sikujua alipokuwepo kwa sababu walinipeleka kwake, walinifunga macho, kitu ambacho halkikufanyika katika mahojiano ya kwanza na ya pili.

Katika mahojiano ya mwisho upekuzi wa kiusalama ulikuwa mkali zaidi na sikuwahi kuruhusiwa kutumia kamera yangu. Waliniambia wana kamera yao na kwamba watapiga picha na kisha watanipatia kanda wa kutumi.

Hawakuniruhusu nirekodi mahojiano hayo.

Walichukua vifaa vyangu vya kazi, lakini walitumia kamera yao, kinasa sauti yao. Na walipomaliza, walinipatia kaseti na kanda ya picha.

Niliwauliza ni kwa nini hawakuniruhusu kutumia kamera yangu na kinasa sauti. Ndipo Ayman al-Zawahri, ambaye pia alikuwepo kwenye mahojiano hayo, alicheka na kusema: “Tunapambana na nchi yenye nguvu sana na hatuamini mtu yeyote.”

“Alaa sawa,” Nilisema, “Naelewa mnahofia naweza kuwaua kwa kutumia kamera yangu .” Walicheka na hapo tukamaliza mkutano wetu.

Tofauti na mahojiano mawili ya kwanza, ambayo yalikuwa marefu sana, ya tatu haikuwa hivyo, kwa sababu ilifanywa katikati ya mashambulio ya Marekani.

Mbali na itifaki za usalama, kulikuwa na chochote kilichobadilika kwa Bin Laden tangu mahojiano mawili ya kwanza?

Nadhani kulikuwa na mabadiliko kidogo katika itikadi yake.

Nilimuuliza maoni yake juu ya watu wengi huko Uropa na Marekani wanaopinga vita huko Afghanistan.

Alichukua msimamo wa kujitetea sana. Alikasirika kidogo na kusema, “Ndio, ndio, uko sawa. Sio Wamarekani wote ni watu wabaya. Kuna watu wazuri wenye mioyo mizuri.”

Kwa hivyo wakati huu alikuwa akiniambia kuwa Wamarekani wote sio watu wabaya.

Nilipomuuliza ikiwa atatafuta suluhisho la kisiasa kwa vita hivyo. Aliniambia kwamba hakuwa akipinga suluhisho la kisiasa.

Wakati mahojiano yalipomalizika tulikunywa chai, mara tukasikia mlipiko wa bomu la bomu. Mlipuko huo ilikuwa ya kutisha na kusema ukweli nilitaka kutoka hapo.

Lakini alikuwa akiongea kwa tabasamu lisilo na uwoga usoni mwake. Alikuwa akifanya kama mtu wa kawaida na kuaniambia: “Angalia, Bwana Mir, kumbuka maneno yangu: Wamarekani siku moja watazungumza na Taliban. Kumbuka maneno yangu.”

Sikumuamini. Lakini Osama bin Laden alitabiri mazungumzo kati ya Taliban na Wamarekani mnamo 2001, Osama bin Laden alitabiri muungano wa Taliban na Iran na China. Alitabiri kuwa Marekani haitakuwa tena nguvu kubwa.

Miaka 20 baada ya 9/11 utabiri huo unatimia. Tupende tusipende.

Mahojiano yako na Osama yaliisha vipi?

Alisema: “Asante sana Bwana Mir. Hatujui ikiwa tutaonana tena.”

Aliwaagiza watu wake wanisaidie kutoka Kabul na walifuata maagizo ya kiongozi wao.

Kulikuwa na kiwanja cha UN nje kidogo, na kituo cha ukaguzi ambapo Taliban walinishika kwa masaa mawili au matatu. Lakini mwishowe waliniacha niende.

Walihitimu PhD ya Uwalimu Wafunza Chekechea
Majaliwa:Nimeridhishwa na hatua ya ujenzi wa SGR