Kocha wa Singida Big Stars, Hans Van Der Pluijm amesema iwe isiwe wachezaji wake watapambania alama tatu muhimu dhidi ya Young Africans kesho Alhamis (Novemba 17), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha Hans ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la Young Africans ametoa tambo hizo alipozungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam leo Jumatano (Novemba 16).

Kocha huyo amesema kikosi chake kimefunga safari kutoka mkoani Singida kwa lengo la kupambana na sio kushiriki kwenye mchezo huo na kupata alama moja ama kupoteza, bali wamejiandaa na kupata alama tatu, japo lolote linawezekana kwenye mchezo wa Soka.

“Kwenye mpira chochote kinawezekana na hakuna kisichowezekana, tumekuwa na siku nzuri, Young Africans hawana siku nzuri labda tunaweza kukatisha mbio zao za kufikia mechi ya 46 ya ligi bila kufungwa.”

“Tumekuja hapa sio kushiriki tu bali kufanya kila liwezekanalo kupata alama tatu.” amesema Kocha Hans

Kwenye Michezo 10 iliyocheza Singida Big Stars imeshinda mitano, sare tatu na kufungwa miwili ikiwa nafasi ya nne ikifikisha alama 18, huku Young Africans iliyocheza michezo tisa imeshinda saba na sare mbili ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Serikali yaitaka LATRA kufanya kazi saa 24
Kaze arithishwa mikoba ya Zahera