Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Harerimana Haruna amesema anaandaa Mpango Mkakati Madhubuti ambao anaamini utakisaidia kikosi chake kuchomoza na ushindi dhidi ya Young Africans katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbeya Kwanza FC inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Young Africans siku ya Jumanne (Novemba 30) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.

Kocha Hererimana amesema maandalizi anayoendelea kuyafanya kwa sasa, ni kuhakikisha mambo yanawaendea vizuri kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.

Amesema kila mchezaji wake amemuandalia mpango mkakati ambao utaiwezesha timu yake kupambana kikamilifu dhidi ya Young Africans ambayo msimu huu imeanza kwa kasi kubwa huku ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 16.

“Ni kucheza mtu na mtu, hakuna kumuangalia mchezaji usoni, hii ni mechi yetu ya kwanza tunayopaswa kupata ushindi nyumbani, nyota wangu lazima watulie wacheze mpira,” amesema Haruna ambaye ni raia wa Burundi.

Mbeya Kwanza FC ilipoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu mwishoni mwa juma lililopita, kwa kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons waliokua nyumbani Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Bangala kuikosa Mbeya kwanza FC
Mbeya Kwanza FC yaandaa ZAWADI NONO