Harmonize amefunguka kinachomkera moyoni kuhusu rapa mpya anayevuma mitandaoni na kwenye mkondo mkuu wa vyombo vya habari, Harmorapa anayefananishwa nae.

Ingawa Harmorapa ambaye kupitia wimbo wake ‘Kiboko ya Mabishoo’ ameonekana kuishambulia timu ya WCB hususan Moze Iyobo aliyemtolea lugha ya ukakasi mtandaoni, Harmonize ameonesha kuumizwa na watu maarufu wanakataa kumsaidia kinda huyo kwenye muziki.

“Naumia napoona baadhi ya wasanii wanamfungia vioo Harmorapa, sio vizuri maana naye anatafuta riziki yake,” Harmonize aliiambia XXL ya Clouds Fm.

Mwimbaji huyo ambaye ametambulisha wimbo wake mpya wa ‘Niambie’ aliongeza kuwa anajiona mwenye heri kwa mtu kupata umaarufu kupitia kufananishwa naye kwani inaonesha jinsi alivyopiga hatua.

Alieleza kumkumbuka Harmorapa walipokutana mara ya kwanza kuwa alimlilia machozi akieleza namna anavyomkubali huku akidai watu wanamfananisha naye, hali iliyomfanya ampe moyo kuwa ipo siku atafanikiwa. Hivyo, amefurahi kuona alipo leo.

Kauli hiyo ya Harmonize inaungana na kauli aliyoitoa Boss wa WCB, Diamond Platinumz hivi karibuni akieleza kuwa Harmorapa anahitaji kupewa sapoti badala ya kukandamizwa kwani naye anatafuta riziki na huenda alihangaika usiku mchana kupata pa kutokea.

Juzi, Harmorapa aliiambia Ala za Roho ya Clouds FM kuwa asingependa kuzungumzia habari za Harmonize kwani anataka kuzungumzia habari zake na wimbo wake mpya aliofanya na mkongwe ‘Juma Nature’.

Rashford kulamba dume au garasa Kikosi cha England?
Mawakili wa Manji wawasilisha ‘ombi’ Mahakama isiisome kesi ya ‘Unga’, isikilize ya Uhamiaji