Harmonize amejibu swali la mtangazaji wa Clouds Fm, Diva aliyetaka kujua uhusiano wake wa sasa na menejementi yake ya zamani ya WCB na kama ameshakamilisha fidia ya Sh 500 milioni aliyotakiwa kulipa ili awe na haki za kutumia kazi alizofanya chini ya lebo hiyo.

Diva aliuliza swali hilo jana usiku wakati Harmonize akiendelea kuwaonjesha ladha ya nyimbo zilizo kwenye Albam yake mpya ya ‘AfroEast’, katika uzinduzi wa albam hiyo uliofana Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Ni kweli haikuwa rahisi, imetumika busara ya ziada kati ya pande zote mbili, menejimenti yangu ya zamani na hii ya sasa hivi ili kumaliza lile deni lililokuwepo. Kwakweli haikua rahisi,

“Nilikuwa nauza hiki naongeza, nauza hiki naongezea. Kwahiyo, nawashukuru kwa kunivumilia nikawa nawalipa kidogokidogo, lakini pia kwa upande wangu… nimelipa yote,” aliongeza.

Harmonize ambaye hakutaka kuendelea kuchimba suala hilo baada ya Diva kutaka kujua kama walifikishana mahakamani, aliwashukuru WCB kwa kumlea na kumuunga mkono hadi kufikia hatua aliyofikia leo.

Mkali huyo wa Bongo Fleva jana alizindua albam yake ya kwanza kwa kishindo, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria akiwemo Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dkt. Tulia Ackson.

Harmonize na H-Baba walimkabidhi rasmi Dkt. Kikwete CD ya Albam hiyo yenye nyimbo 18.

Pamoja na hao walikuwepo watu maarufu na mashuhuri ambao walionesha ‘kuupiga salute’ uzinduzi wa albam hiyo uliojaa ubunifu.

CORONA: Wayne Rooney adai Serikali imewafanya wachezaji kama ‘wanyama’
Video: Kumlipia mfungwa faini ni kuunga mkono kosa?