Mwimbaji anaeunda kundi la WCB, Harmonize ameeleza baadhi ya matatizo mazito aliyowahi kuyapitia katika harakati za kusaka tonge, ikiwa ni pamoja na hatari iliyokuwa mbele yake ya kusulubiwa na wananchi wenye hasira kali katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Msanii huyo ambaye hivi karibuni ameachia kombora lake la ‘Matatizo’ likiwa na video inayoonesha matukio mbalimbali, amesema kuwa sehemu ya kipande cha video hiyo kimeonesha tukio hilo.

Mkali huyo ameeleza kuwa katika video hiyo, kuna sehemu anaonekana anauza maji halafu anatokeo mteja mwenye gari aina ya IST ambaye baada ya mazungumzo kidogo Harmonize anaonekana akiikimbiza gari hiyo kwa mguu, ni tukio la kweli lililozua hatari ya maisha yake.

Alisema mtu huyo alikuwa msichana aliyekuwa anaendesha gari hiyo alitaka amuuzie maji katika barabara ambayo taa nyekundu ilikuwa imesimamisha magari ya upande huo lakini baada ya kumpa maji kwa bahati mbaya taa ya kijani iliwaka na kuruhusu magari kuondoka, na msichana huyo akalazimika kuondoka kabla ya kulipia maji.

“Niliikimbiza lile gari lakini likaniacha, lakini kufika mbele ilisimamishwa tena kwahiyo nikaweza kumfikia huyo msichana. Sasa alikuwa amefunga vioo nikaanza kumgongea ili afungue anipe pesa yangu, aisee yule msichana alipiga kelele ‘Mwizii… mwiziii…mwizii’,” Harmonize alisimulia katika kipindi cha Jahazi cha Clouds Fm.

Alisema baada ya kuona balaa hilo na kwa kutambua kuwa pale ni ‘Kariakoo’, aliondoka haraka na kuiacha riziki yake ikitokomea.

Hata hivyo, imebaki story tu. Maisha yamebadilika, hivi sasa Harmonize yuko na mrembo maarufu ambaye hata hakumuota enzi hizo, Jackline Wolper na huenda yule aliyempigia ‘yowe za mwizi’ ni shabiki yake mkubwa.

Hakuna aijuae kesho hata mtunzi wa kalenda. Endelea kuikimbiza ndoto yako!

Mnyika ajibu kuhusu taarifa za kumkataa Lowassa, Kuhama Chadema
Lowassa afunguka kuhusu hali ya Siasa nchini, awapa Chadema ‘ukweli mchungu’