Mshambuliaji wa klabu ya Tottenham Hotspurs Harry Kane ameondolewa kwenye kambi ya timu ya taifa ya England baada ya kushindwa kufaulu vipimo vya utimamu wa mwili.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, aliitwa kwenye kikosi cha timu hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya kurejea uwanjani kuitumikia klabu yake ya Spurs ambayo ilimkosa kwa muda mrefu kufuatia majeraha ya kifundo cha mguu.

Kane amecheza dakika 73 tangu aliporejea uwanjani, baada ya kupatwa na majeraha hayo wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England dhidi ya Sunderland Septemba 18.

Kocha  wa  muda wa timu ya taifa ya England Gareth Southgate amethibitisha kumuondoa Kane, na anaamini atakua fit katika siku zijazo ambapo atakiita tena kikosi chake kwa ajili ya kuendelea na kampeni za kuwania kusaka nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia.

Mwishoni mwa juma lililopita kikosi cha England kilicheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya majirani zao Scotland, na Kane hakuwa sehemu ya timu hiyo.

Kikosi cha England kwa sasa kinajiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa dunia mwaka 2010, timu ya taifa ya Hispania ambao utachezwa kesho katika uwanja wa Wembley.

Memphis Depay: Sifahamu Chochote Kuhusu Mustakabali Wangu
Memphis Depay Aiangusha Luxembourg