Licha ya meneja wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich Niko Kovac kutangaza msimamo wa kutoafiki suala la kuuzwa kwa beki Jerome Boateng katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, klabu ya  Manchester United imeendelea kuwa na matumaini ya kumsajili mchezaji huyo hata kwa njia ya mkopo.

Kwa mujibu wa taarifa zilziotolewa na kituo cha televisheni cha Sky Sports, meneja wa Man Utd Jose Mourinho anaushinikiza uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha beki huyo anasajiliwa kabla ya kufungwa kwa dirisha baadae hii leo.

Mourinho anaamini beki huyo atakua msaada mkubwa katika kikosi chake, ambacho kitaanza kampeni ya kusaka ubingwa wa England kesho Ijumaa kwa kucheza na Leicester City kwenye uwanja wa Old Trafford.

Hata hivyo bado haijafahamika kama uongozi wa klabu ya Man Utd umeshatuma ofa ya kumsajili beki huyo, ili kuwahi muda wa saa kadhaa uliosalia kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Awali Man Utd walikua na mpango wa kumsajili beki kutoka nchini Colombia Yerry Mina akitokea kwa mabingwa wa Hispania FC Barcelona, lakini dili hilo limefeli kutoka na mchezaji huyo kufanikisha mpango wa kujiunga na Everton.

Mchezaji mwingine anaecheza nafasi ya ulinzi ambaye anapewa nafasi kubwa ya kujiunga na Man Utd kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili ni Harry Maguire wa klabu ya Leicester City.

Tarifa zinaeleza kuwa usajili wa Maguire haupewi kipumbele na meneja Jose Mourinho, na badala yake viongozi wa Man Utd wakiongozwa na mtendaji mkuu Ed Woodward, wamekua wakishinikiza dili hilo, kwa kuamini huenda akasaidia katika safu ya ulinzi.

Mpaka sasa chaguo la kwanza la Mourinho ni beki Boateng, ambaye anaamini ana vigezo vyote vya kuwa mchezaji atakaesaidia katika safu yake ya ulinzi.

Boateng mwenye umri wa miaka 29, amekua katika changamoto za kupata majeraha kwa muda mrefu, hali ambayo ilimfanya acheze michezo 27 ya ligi ya Ujerumani  Bundesliga, tangu Disemba 2016.

Msimu uliopita alikabiliwa tena na majeraha ya nyama za paja, na alishindwa kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kilichoshiriki fainali za kombe la dunia zilizofanyika nchini Urusi.

Beki huyo pia anatarajiwa kukosa michezo ya mwanzoni mwa msimu ujao, kutokana kuhitaji kuwa na mazoezi ya kutosha, baada ya kupona jeraha la nyama za paja.

Alifanikiwa kurejea mazoezini mwezi uliopita, na alikua miongoni mwa wachezaji walioanzia benchi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya FC Rottach-Egern uliochezwa jana Jumatano. Bado ana mkataba wa FC Bayern Munich hadi mwaka 2021.

Rais Durtete atishia kuwaua Askari Polisi 102
Mambo 5 usiyotakiwa kufanya mara baada ya kula

Comments

comments