Uongozi wa klabu ya Arsenal, huenda ukafanya mabadiliko katika benchi la ufundi mwishoni mwa msimu huu, endapo hautoridhishwa na kazi ya mzee Arsene Wenger ambaye mwishoni mwa msimu uliopita alisaini mkataba mpya wa miaka miwili.

Uongozi wa klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London, umepanga kufanya tathimini ya kina kuhusu mwenenndo wa mzee huyo kutoka nchini Ufaransa, baada ya kuona hali sio nzuri katika kikosi chao msimu huu.

Taarifa iliyochapishwa na kwenye gazeti la Daily Mail ya nchini England, imeeleza kuwa, uongozi wa The Gunners haukutarajia matokeo yanayopatikana hivi sasa, kufuatia imani kubwa waliyoiweka kwa babu huyo aliyedumu kwa kipindi cha miaka 20 tangu alipoajiriwa klabuni hapo.

Taaifa hiyo imeongeza kuwa, The Gunners tayari wameshaanza kuandaa orodha ya makocha wa kuwatathmini katika kumpata mbadala wa Wenger kama itaamua kuachana naye mwishoni mwa msimu.

Kocha wa Monaco, Leonardo Jardim, kocha wa Ujerumani, Joachim Low, kocha Mkuu wa Celtic, Brendan Rodgers na kocha wa Manchester City, Mikel Arteta ni miongoni mwa watu awali walioorodheshwa.

Hata hivyo kama tathmini itakayofanywa mwishoni mwa msimu huu itaridhisha, Wenger ambaye nafasi yake iko hatarini baada ya kipigo cha Jumapili katika fainali ya Carabao Cup kutoka kwa Manchester City, atalazimika kupambana ili kumalizia miezi yake 12 ya mkataba wake.

Lakini inavyoonekana sasa ndani ya Arsenal nguvu ya kumng’oa Wenger klabu hiyo ya Kaskazini mwa London mwishoni mwa msimu ni kubwa.

Tathmini ya mwishoni mwa msimu ndio itabeba mustakabali wa Wenger kama apewe nafasi nyingine ya kubaki kwa msimu mwingine au aondolewe. Hii inamuacha apambane maswali magumu juu ya nini amevuna katika msimu hadi sasa.

Zaidi itategemea kama ataiwezesha timu kupata nafasi ya kurejea kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu, ingawa hiyo bado haitatosha kuwa sababu ya kumbakiza.

Na safari ya kurejea kwenye michuano hiyo mikubwa ya Ulaya inaonekana kuwa ngumu, kwa sasa The Gunners wakizidiwa pointi 10 na Tottenham Hotspur wanaoshika nafasi ya nne.

Hivyo, nafasi nzuri zaidi ya Arsenal kurejea kwenye michuano hiyo kwa kushinda taji la UEFA Europa League, ingawa wanakabiliwa na mtihani mgumu wa kumenyana na AC Milan katika raundi ijayo, hatua ya 16 Bora.

Serikali kutoa chanjo ya saratani kwa watoto wa kike
Kilio cha Young Africans chasikika