Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chaumma, Hashim Rungwe amesema kuwa chama chake kitafungua shauri mahakamani ili kupata tafsiri ya kisheria kuhusu kutohojiwa mahakamani kwa matokeo ya rais baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mshindi.

Akiongea na waandishi wa habari jana, Rungwe alieleza kuwa wanahitaji kupata tafsiri na muongozo kuhusu kifungu cha katiba kinachozuia kuhojiwa mahakamani kwa matokeo ya rais ikiwa nchi hii ni ya kidemokrasia.

“Na haya mambo ya matokeo ya rais tunayafikiria namna ya kufanya ili twende mahakamani. Mahakama itupe tafrisiri ina maana gani? Kwamba hata kama mtu ana malalamiko basi wakae nayo tu bila kuwa na jibu lolote katika nchi ya kidemokrasia,” alisema.

“Watu lazima waende mahali, na vyombo vya juu vilivyopewa mamlaka waseme tunafanyaje? Lakini hatuwezi kukaa kimya tu. Kwa hiyo sisi tunaelekea mahakamani kuomba mahakama iingilie kati ili watu wajue na sisi tupate majibu,” aliongeza.

Hashim Rungwe hakusaini fomu za matokeo ya urais alizokabidhiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya kumtangaza Dkt. John Magufuli kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hali iliyodhihirisha kuwa hakukubaliana na matokeo hayo.

 

Hiki Ndicho Rais Kagame Amemuandikia Rais Mteule Dkt. Magufuli
Tanzania Ya Viwanda Kuanza Rasmi Leo, Dunia Kushuhudia Kiapo Cha Magufuli