Mchezaji Hassan Isihaka hatimaye amerejea kundini kujiunga na wenzake baada ya kumaliza muda wake wa kuitumikia adhabu ya kusimamishwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kwa sababu ya utovu wa nidhamu,baada ya kumgomea kocha Jackson Mayanja aliyemtaka kucheza mechi ya kombe la shirikisho dhidi ya Singida United.
Mlinzi huyo alizua tafrani katika mchezo huo na uongozi wa Simba kuja juu na kulipeleka suala lake kwenye kamati ya utendaji iliyotoa adhabu hiyo ya kusimama kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Hivi karibuni kocha Jackson Mayanja ameonekana hataki mchezo kwa wachezaji wake kuwa na vitendo vya nidhamu kwa madai kwamba kitendo hicho ni kama wachezaji wanataka kumpanda kichwani kocha wao.
Mbali na Isihaka, mchezaji mwingine aliyekumbwa na balaa la kusimamishwa ni Abdi Banda ambaye naye alifanya kitendo kama hicho cha kumgomea kocha Mayanja lakini safari hii ilikuwa katika mchezo dhidi ya wagosi wa kaya Coast Union uliopigwa mkoani Tanga na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mayanja aliyejiunga na Simba akitokea klabu ya Coast Union ya Tanga, amekuwa mbogo kwa kipindi hiki kutaka kuwanyoosha wachezaji wake wenye nidhamu mbaya kurudi kwenye mstari na kuendelea kufanya kazi ya kucheza mpira iliyowaleta kwenye klabu hiyo.
Hata hivyo klabu ya Simba inaonekana itamrejesha haraka Abdi Banda kutokana na ukweli kwamba klabu hiyo ingepata wakati mgumu katika safu ya ulinzi katika mchezo unaofuata wa ligi kuu dhidi ya Toto Africans ya Mwanza kwa kuwa mlinzi wao Mganda Juuko Murshid anatumikia adhabu ya kadi.