Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa hata yeye pia hawatambui CUF upande wa Katibu Mkuu wa CUF. Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuwa watu hao hawatambuliki kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusiana na mambo mbalimbali ya bunge na kusema kuwa hawezi kumtambua Katibu Mkuu wa CUF,  Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuwa mtu huyo hatambuliki kwa msajili hivyo yeye ataendelea kumtambua Profesa Lipumba pamoja na Magdalena Hamis Sakaya kwa kuwa ndiyo watu wanaotambulika katika vyombo husika.

“Mimi sina tatizo lolote na chama cha siasa ila ni masuala ya utaratibu tu mwenye kumbukumbu ya vyama vya siasa na katiba za vyama vya siasa na viongozi halali wa vyama vya siasa ni msajili wa vyama vya siasa siyo mtu mwingine yoyote kwa hiyo linapotokea jambo la chama ambacho kina mvutano kazi yangu mimi ni kumuuliza huyo ambaye ndiyo muweka hazina wa vyama vya siasa ambaye ni msajili, akisema si mtambui na mimi nakuwa simtambui, akisema namfahamu basi na mimi nakuwa namfahamu lazima twende kwa utaratibu,”amesema Ndugai

Aidha, Spika Ndugai amesisitiza kwa kusema kuwa yeye hawezi kuibuka na kuanza kuwatambua watu ambao hawatambuliki kwa msajili wa vyama vya siasa nchini na kusema kuwa kwa kufanya hivyo atakuwa anakiuka utaratibu ambao upo na inaweza kuleta shida zaidi.

Hata hivyo, Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi yeye anamtambua Mwenyekiti wa CUF Taifa kuwa ni Profesa Ibrahim Lipumba na kumtambua Magdalena Hamis Sakaya kama Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF.

Video: Diamond, Rayvanny, Harmonize, Rich Mavoko kwenye 'Zilipendwa', Itazame hapa
Pacquiao aungana na 'Timu Mayweather', amshusha McGregor