Madaktari Bingwa wazawa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete JKCI kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (Aorta) uliokuwa umetanuka pamoja na valvu yake (Aortic valve insufficiency) bila ya usimamizi wa madaktari kutoka nje baada ya miaka kadhaa ya kujifunza upasuaji huo kutoka kwa wataalam wenzao wanaofika JKCI kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.

Upasuaji huo unaojulikana kwa jina la kitaalamu Bentall Surgery  ulichukua masaa matano kukamilika ambapo kwa sasa mgonjwa anaendelea vizuri na anatarajia kuruhusiwa wakati wowote kuanzia sasa.

Mgonjwa alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifua na baada ya uchunguzi aligundulika kuwa mshipa mkubwa wa damu (aorta) unaotoa damu kutoka kwenye moyo na kusambaza damu mwili mzima umepanuka sana na valvu yake ya moyo inavuja damu.

Akizungumzia upasuaji huo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa (JKCI) Dkt. Godwin Sharau amesema  tatizo hilo mara nyingi huwapata watu wengi wenye umri wa kuanzia miaka ya 50 kwenda juu lakini pia uwapata watu wanaosumbuliwa na shinikizo la damu la muda mrefu hivyo mshipa huo kupoteza umahiri wake wa kuweza kustahimili presha.

Dkt. Sharau ambaye pia ni Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto alisema kwa mgonjwa ambaye hatapata matibabu husika kwa wakati mshipa huo huendelea kutanuka na hivyo kupelekea kufa ghafla.

“Kwa miaka mingi upasuaji wa Bental operation kwa hapa JKCI umekuwa ukifanyika lakini chini ya usimamizi wa madaktari wenzetu kutoka nje ya nchi, sasa wataalam wetu wameonesha umahiri mkubwa wa kufanya upasuaji huu, hii ni hatua nzuri sana katika Taasisi yetu”, Amesema Dkt. Sharau.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya upasuaji watu wazima wa (JKCI) Dkt. Evarist Nyawawa amesema mgonjwa huyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina ilionesha yakuwa mshipa mkubwa wa damu (Aorta) ulikuwa umetanuka kiasi cha kwamba muda wowote ungeweza kupasuka.

Naye Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (aorta) uliotanuka pamoja na valvu yake (Bental operation) Benny Mongi aliwashukuru  wataalamu hao wa JKCI na kuwapongeza kwa kutumia utaalam wa hali ya juu waliokuwa nao kwa kuokoa maisha yake.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja wa Oktoba hadi Novemba 2021 madaktari wazawa mabingwa waupasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (aorta) uliokuwa umetanuka pamoja na valvu yake (Aortic valve insufficiency) bila ya usimamizi wa madaktari kutoka nje ya nchi kwa mgonjwa mmoja na upandikizaji wa mishipa ya damu ya moyo bila ya kusimamisha moyo kwa wagonjwa watatu.

Waziri wa ulinzi afutwa kazi Msumbiji
Bilioni 67.6 kunufaisha vikundi vya kinamama