Beki wa kulia wa kikosi cha Arsenal Hector Bellerin, atakua nje ya uwanja kwa muda wa majuma manne, kufuatia majeraha ya kifundo cha mguu alioyapata wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England dhidi ya Tottenham Hortspurs.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 21 alitarajiwa huenda angewahi mchezo wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Man Utd, lakini imethibitika bado anakabiliwa na maumivu.

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger, amethibitisha taarifa za beki huyo kuendelea kukaa nje ya kikosi chake, alipozungumza na waandishi wa habari muda mchache uliopita kuhusu mchezo dhidi ya Man Utd.

“Aliumia sekunde 10 za mwisho katika mchezo dhidi ya Spurs Novemba 06, baada ya kujaribu kumzuia Danny Rose,” Alisema Arsene Wenger.

Bellerin, ambaye tayari ameshacheza michezo 11 akiwa na kikosi cha kwanza cha Arsenal msimu huu, huenda akakosa michezo minane, ukiwepo dhidi ya mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris St-Germain.

Mchezo mwingine ambao beki huyo kutoka nchini Hispania ataukosa ni dhidi ya FC Basel (Disemba 06), Southampton (Kombe la ligi EFL) utakaochezwa Emirates Stadium, Novemba 30.

Wakati huo huo Arsene Wenger, amesema mshambuliaji Alexis Sanchez anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kesho, ili kupata uhakika wa kumtumia kwenye mchezo dhidi ya Man Utd siku ya jumamosi.

Sanchez alicheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Uruguay ambao walikubali kichapo cha mabao matatu kwa moja.

Mshambuliaji huyo aliripotiwa kuumia kiazi cha mguu mwanzoni mwa juma lililopita na alikosa mchezo wa timu yake ya taifa dhidi ya Colombia.

Mbeya City FC Wajiweka Mbali Na Mitandao Ya Kijamii
Mayweather amtembelea Trump