Uongozi Mpya wa Young Africans chini ya Injinia Hersi Said umemtangaza Saad Kawemba kuwa Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu hiyo sambamba na kumtaja Walter Harson kuwa Meneja mpya wa Kikosi chao.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo, Saad Kawemba amepewa majukumu hayo baada ya aliyekuwa kwenye nafasi hiyo, Thabith Kandoro kumaliza mkataba wake.

Walter Harson ambaye alikuwa ni Katibu Mkuu Mtendaji wa Klabu ya KMC FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, amechukua nafasi ya Hafidh Saleh aliyepangiwa majukumu ya kuwa Mratibu wa Timu.

Uteuzi wa viongozi hao wawili umeanza rasmi leo Jumatatu (Agosti Mosi), ambapo kikosi cha Young Africans kinaendelea na Maandalizi ya mchezo wa Wiki ya Mwananchi sambamba na Msimu Mpya wa 2022/23.

Tayari Young Africans imezindua rasmi Wiki ya Mwananchi leo Jumatatu (Agosti Mosi), huku ikiunda Kamati yenye Wajumbe Saba wakiongozwa na Mwenyekiti Arafat Haji ambaye ni Makamu wa Rais wa Klabu hiyo.

Wajumbe wa Kamati hiyo ni Wakili Simon Patrick, CPA. Haji Mfikirwa, Taji Liundi, QS. Said Yassin Mrisho, Khamis Abeid Dacota na Christinah Oscar Korosso.

Kilele cha Wiki ya Mwananchi kinatarajiwa kuwa Jumamosi ya Agosti 6, 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Try Again amshukuru Tarimba, SportPesa
Wazuia msafara wa Waziri kumpa kero ya maji