Mbunge wa Jimbo la Ulanga kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Goodluck Mlinga amesema kuwa Ndege aina ya Airbus 380, EK701 ya Shirika la Ndege la Emirates si ya kwanza yenye ukubwa huo kutua nchini kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka 2018/19, ambapo amesema kuwa ndege kubwa ya kwanza kutua nchini ni aina ya Antonov mwaka 2009 ikiwa imepakia mitambo ya kufua umeme ya Richmond.

“Ndege iliyokuja kipindi kile ilikuwa inaitwa (Antonov) ilikuwa na tani 285 wakati hii iliyokuja jana ina tani 276, iliyokuja kipindi kile ilikuwa na injini sita, wakati iliyokuja jana ina injini nne, Ndege hii iliyoleta mitambo ya Richmond ilikuwa na urefu wa mita 80, wakati hii ina urefu wa mita 76,”amesema Mlinga

Aidha, Ndege ya Shirika la Emirates iliyokuwa ikielekea Mauritius ilitua kwa dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA) kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya nchini humo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania ( TCAA), Hamza John amesema kuwa ni mara ya kwanza kwa ndege aina ya ‘Airbus’ yenye ukubwa huo kutua nchini.

Meek Mill aachiwa huru
Chadema wadai hawahusiki na maandamano