Nchi za Hispania na Ureno zimeanza kuishawishi Morocco kuwasilisha ombi la pamoja la kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 2030.

Taarifa zilizotoka ndani ya serikali ya Hispania zinadai kuwa, mpango wa kuishawishi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, umeandalia vilivyo na inaamika utakubaliwa vyema na shirikisho la soka la Morocco sambamba na serikali yao.

Tayari waziri mkuu wa Hispania Pedro Sanchez ameshafanya ziara kwenye mji mkuu wa Morocco (Rabat), sambamba na kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo Saadedin Al Othmani pamoja na Mfalme King Mohamed VI kwa ajili ya kushawishi jambo hilo.

“Nimeshawasilisha pendekezo kwa serikali ya Morocco kwa ajili ya kushirikiana kuandaa fainali za kombe la dunia, ninaamini linafanyiwa kazi na litakubalika kwa asilimia zote,” alisema Sanchez alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari.

“Tunaamini kwa pamoja nchi hizi tatu zikifanikisha mpango wa makubaliano na tukawasilsiha ombi la kuwa mwenyeji wa fainali za 2030, itakua rahisi kushinda kutokana na uzoefu tuliojifunza kwa wenzetu waliojaribu kufanya hivyo na wakafanikiwa.”

Hispania wamewahi kuwa wenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 1982, na walijaribu kuomba kuwa wenyeji kwa kushirikiana na Ureno kwa ajili ya fainali za mwaka 2018, lakini walishindwa na nafasi hiyo ikaenda Urusi.

Ureno hawajawahi kuandaa fainali za kombe la dunia, lakini waliweza kuwa wenyeji wa fainali za mataifa ya Ulaya mwaka 2004, na timu yao ilifika hatua ya fainali na kufungwa na Ugiriki bao moja kwa sifuri.

Mara kadhaa Morocco wamekua wakijaribu kuomba kuandaa fainali hizo, lakini wamekua wakishindwa katika hatua ya kupigiwa kura kwenye mkutano mkuu wa FIFA.

Waliwahi kuomba kuwa wenyeji wa fainali za 2006, 2010 na 2026 ambapo nafasi hiyo ilichukuliwa na nchi za Marekani, Mexico na Canada ambazo zitaandaa kwa pamoja.

Kama mpango wa Hispania, Ureno na Morocco utakubalika na kupigiwa kura kwenye mkutano mkuu wa FIFA, fainali za kombe la dunia zitaweka historia ya kuchezwa kwenye mabara mawili tofauti kwa wakati mmoja tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930.

Video: Dkt. Bashiru Ally afunguka kuhusu vyama vya siasa kutoshirikiana
Zomea zomea yamkera Leonardo Bonucci