Kufuatia malalamishi ya wakenya katika mitandao ya kijamii kuhusiana na miili 19 iliyoopolewa mto Yala, shirika la haki za kibinadamu la Haki Afrika limeelekea katika kaunti ya siaya ili kufuatilia tukio hilo na kampeni inaendelea mitandaoni wakenya wakionyesha ghadhabu zao.

Mwanaharakati Boniface Mwangi, akiwa pamoja na mkuu wa shirika la Haki Afrika, Hussein Khalid, wamehesabu zaidi ya miili 20 iliyooza katika chumba cha kuhifadi maiti katika Hospitali ya Yala na wameendelea kuwalaumu polisi na kuwatuhumu kama wahusika wakuu wa mauaji ya raia kiholela.

Linasema kwamba liligundua miili 21 katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya kaunti , ambapo miili mingi ilikuwa imefungwa kamba na mingine kupatikana katika magunia, mingine ikiwa na alama za kukatwa na mingine ikiwa imefungwa na nailoni katika vichwa.

Shirika hilo linasema kwamba lilithibitishiwa na kituo hicho cha kuhifadhia maiti kwamba mnamo mwezi Oktoba kilizika miili tisa katika kaburi la pamoja.

Haki Afrika imesema kwamba muogeleaji ambaye amekuwa akiopoa miili hiyo amesema kwamba tangu mwezi Julai 2021, aliopoa miili 31 miili kumi ikiwa ndani ya gunia na wanaharakati hao walithibitisha miili miwili iliokuwa ikielea katika maji ya mto huo ambayo pia hutumika kwa matumizi ya nyumbani na jamii za eneo hilo na ameongezea anaamini kwamba huenda kuna miili zaidi inayooza katika mto huo.

Shirika hilo la haki za kibinadamu hivi sasa limetoa wito wa kutaka kubaini miili hiyo. Vilevile limeitaka serikali kufichua ni nani anayehusika na mauaji hayo na kutupwa kwa miili hiyo katika mto huo ili kuchukuliwa hatua kali.

Kamanda wa polisi eneo la Gem, Charles Chacha alithibitisha kuongezeko kwa visa vya miili kupatikana Mto Yala akisema kuna miili 20 ya watu wasiojulikana katika makafani ya Hospitali ya Yala ambapo 19 kati ya hiyo iliopolewa kutoka Mto Yala, saba ikpatikana karibu na maporomoko ya Ndanu.

Kibao kinachoonyesha chumba cha kutunzia maiti cha hospitali ya Yala

Afisa Mkuu wa Matibabu katika hospitali hiyo, Bruno Okal alisema miili hiyo imekuwa ikipelekwa katika mochwari kwa muda wa miezi mitatu iliyopita na polisi na sasa watazika miili hiyo katika kaburi la pamoja kwa kuwa hakuna jamaa waliojitokeza kuitambua na kuichukua.

Wakazi wa eneo hilo waliohojiwa na wanahabari walisema kuwa miili hiyo inaletwa kutoka maeneo tofauti ya nchi ikiwa ndani ya gari na kutupwa mtoni na wengine walisema kuwa miili hiyo huletwa kwa gari aina ya pick-up nyeusi na mara nyingine kwa Probox usiku wa manane ama alfajiri.

Katika taarifa iliyoandikwa Jumatano, Januari 19, na kutiwa saini na msemaji wa polisi, Bruno Shioso, ilibainika kuwa kitengo maalum kilikuwa kimeundwa kuchunguza suala hilo ikiongozwa na timu ya maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imeanza uchunguzi wao na itafumbua kitendawili cha idadi kubwa ya miili hiyo.

“Kikosi kutoka afisi ya mKurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kiliteuliwa na kupewa jukumu la uchunguzi ambao umekuwa ukiendelea kuhusu matukio hayo,” ilisema taarifa hiyo.

Maji ya Mto Yala hutumika kwa matumizi ya Binaadamu

Zaidi ya hayo, Idara ya polisi ilisema kuwa timu nyingine ya wataalam wa uchunguzi walikuwa wametumwa katika eneo hilo kusaidia katika uchunguzi.

Shioso alisema kuwa kikosi hicho kitasaidia katika utambuzi wa miili ambayo haijadaiwa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Yala Sub County Level IV.

“Ili kuharakisha utambuzi wa waathiriwa na uchunguzi mwingine wa kisayansi, timu maalum ya uchunguzi wa kisayansi kutoka makao makuu ya DCI imetumwa katika eneo la tukio huko River Yala na hospitali ya Tala Sub County Level IV kusaidia uchunguzi zaidi,” ilisema taarifa hiyo.

Kupatikana kwa miili hii kiholela kumetafsiriwa na duru za kijamii kama kuzorota kwa hali ya usalama nchini Kenya ambako kumefikia kiwango cha hatari hasa kutokana na ongezeko la visa vya watu kutoweka kisha kupatikana wameuawa.

Makonda kitanzini kwa Jinai
Kaligraph Jones kurejea shuleni