Meneja wa mabingwa watetezi Ligi Kuu ya England Manchester City, Pep Guardiola ameingia hofu, kufuatia jeraha linalomkabili mshambuliaji wake kutoka Argentina, Sergio Kun Aguero.

Aguero alipata majereha ya goti akiwa kwenye mpambano wa ligi ya EPL dhidi ya Burnley jana usiku, na inahisiwa huenda ameumia kwa kiasi kikubwa.

Mshambuliaji huyo alicheza kwa dakika 45 tu kwenye mchezo huo dhidi ya Burnley, na baada ya hapo akaumia na nafasi yake kuchukuliwa na Gabriel Jesus.

Guardiola alisema: “Haonekani kuwa sawa, goti lake lina tatizo, tutaona kesho (Jumanne), baada ya uchunguzi.  Alikuwa akipambana tangu mwezi uliopita  kuhusu maumivu katika goti lake, tutaona.”

Alipoulizwa ikiwa ana wasiwasi Aguero atakosa michezo iliyosalia ya msimu huu, Guardiola alijibu itategemeana na vipimo vya mwisho.

“Kesho (Jumanne) tutaona. Mimi sio daktari, lakini haonekani kuwa sawa,” alisema Guardiola

Kuumia kwa Aguero kunaiweka City katika wakati mgumu kwenye harakati zao za kuwania mataji tofauti wanayoshiriki msimu huu.

Wakati wakiwa na uwezekano finyu wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England, City bado wapo katika mbio za kuwania mataji mawili ambayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA.

Ikumbukwe tayari msimu huu, City wameshatwaa taji moja ambalo ni Kombe la Ligi. Taji hilo walitwaa Machi baada ya kuifunga Aston Villa anayoichezea nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta kwenye uwanja wa Wembley.

Kwa mujibu wa ratiba yao, Manchester City wata wataenda Stamford Bridge kuumana na Chelsea kwenye mchezo wa Ligi, Alhamisi kabla ya safari ya kuelekea Newcastle kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA Jumapili.

Lakini pia watakuwa na mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real unaotarajiwa kuchezwa kati ya Agosti 7 au 8.

Mastaa FC Barcelona watibuana, kocha aingilia kati
Video: Waziri Mwakyembe "SADC inatambua mchango wa wanahabari katika janga la covid 19"