Wananchi jijini Mwanza wamekumbwa na taharuki na hofu kufuatia vifo vya nguruwe takribani 3000 kwa kipindi kifupi kutokana na ugonjwa wa homa ya nguruwe.

Kutokana na idadi hiyo kubwa ya vifo vya nguruwe vinavyotokana na ugonjwa huo, wananchi wengi wamekuwa na hofu ya kuambukizwa ugonjwa huo wakiufananisha na ugonjwa hatari wa homa ya mafua ya nguruwe ulioitikisa dunia.

Baadhi ya wananchi walieleza kuwa wamesitisha kula nyama ya nguruwe maarufu kama ‘kitimoto’  wakihofia kuambukizwa ugonjwa huo huku wafanyabiashara wa nyama hiyo walilalamikia kuporomoka kwa soko.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Mifugo Mkoa wa Mwanza, Yohana Segenge aliwatoa wasiwasi wananchi kwa kueleza kuwa ugonjwa wa homa ya nguruwe uliopo jijini humo ni tofauti na ugonjwa wa mafua ya nguruwe.

Dk. Segenge alieleza kuwa ugonjwa wa homa ya nguruwe haumuambukizi binadamu kwa namna yoyote tofauti na ugonjwa wa mafua ya nguruwe ambao humuambukiza binadamu.

“Ugonjwa huu wa homa ya nguruwe unaenezwa kwa njia ya virusi, na hivi virusi vinashambulia mifugo aina ya nguruwe, nguruwe pori na nguruwe wanaofugwa. Ugonjwa huu hauambukizi binadamu na wala hauna madhara yoyote kwa binadamu. Kwa hiyo nachosema, wananchi wasiwe na hofu bado nyama ya nguruwe ni salama,”alisema Dk. Segenge.

Jiji la mwanza linakadiriwa kuwa na nguruwe zaidi ya 56,000.

Kilichojiri Baada Ya Vigogo Wa TRA Wa Makontena Kuomba Dhamana Mahakama Kuu
Makonda Awatumia Salamu Wanaoishi Mabondeni, Awataka Wasiichokoze Serikali