Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim M. Majaliwa amewapongeza viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa usimamizi mzuri uliopelekea kumalizika kwa ujenzi wa ofisi hiyo  kwa wakati iliyopo mji wa serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Ameyasema hayo jijini Dodoma mara baada ya kutembelea jengo jipya la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililopo kwenye mji wa serikali, eneo la Mtumba jijini humo.

Amesema kuwa, ameridhishwa na kiwango cha ujenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliyojengwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu na kwa gharama nafuu ya kiasi cha shilingi bilioni moja iliyotengwa na serikali.

“Serikali imekuwa ikifuatilia hatua zote za ujenzi katika mji wa serikali ili kuhakikisha ujenzi unafanywa kwa viwango, na jengo la Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora limekuwa likienda vizuri sana katika hatua zote” amesema Majaliwa.

Aidha, amesema kuwa anatambua kwamba Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora imeshafanya uzinduzi wa jengo lake, jambo ambalo ni jema na limeonyesha namna ambavyo ofisi hiyo imetekeleza vema maelekezo ya serikali.

Pia, Majaliwa ameweka bayana kuwa, uzinduzi rasmi wa Ofisi zote zilizojengwa kwenye mji wa serikali utafanywa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika tarehe rasmi atakayoipanga.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim M. Majaliwa kwa kutenga muda wake kuitembelea Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora katika mji wa serikali, na kumshukuru kwa namna alivyowahimiza mawaziri kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa ofisi zao kwenye mji wa serikali ili ukamilike kwa wakati.

Naye Kaimu Meneja wa Wakala ya Majengo Tanzania (TBA), Herman Tanguye amesema kuwa, Wakala ya Majengo Tanzania imekamilisha ujenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa asilimia 99.5% kwa muda uliopangwa na kwamba hatua iliyobakia ni kukamilisha mandhari ya nje ya ofisi.

 

Kamwe CUF haiwezi kufa, 'Waliohama ni wasaliti- Khalifa
Vijana watakiwa kuwa wazalendo kwa nchi yao

Comments

comments