Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imetoa ufafanuzi kufuatia ujumbe wa sauti ya Mbunge wa Nzega Mjini, Dkt. Hamisi Kigwangalla unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambao pamoja na mambo mengine anataka huduma ya kujifukiza iliyoanzishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuvunjwa kwa kuwa inaleta picha mbaya.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano MNH, Aminieli Aligaesha leo April 4, 2021 imeeleza kuwa ugonjwa wa Covid 19 ni ugonjwa mpya ambao hadi sasa duniani hakuna mwenye majibu sahihi.

“Majibu sahihi yanatokana na tafiti zinazofanywa sehemu mbalimbali duniani kwa sasa. Tafiti hizi zinaanza na wazo ambalo wataalamu wanalifanyia kazi kisayansi na kutoa majibu. Kwa muda kumekuwa na taarifa kuwa tiba asilia ikiwemo kujifukiza kunasaidia katika tiba ya Covid 19,” imeeleza taarifa hiyo ya ufafanuzi.

Aidha, MNH imeeleza kuwa tafiti mbalimbali kutoka sehemu nyingine duniani kama Israel na Italia zimeongelea kujifukiza (steam therapy) kama njia mojawapo ya tiba ya ugonjwa huu na mengine ya upumuaji, hivyo MNH iliona kuna umuhimu wa kuleta huduma hiyo ili wananchi walio tayari waitumie na pia wataalamu wapate nafasi ya kuifanyia utafiti kwa njia za kisayansi na kutoa majibu sahihi iwapo inafaa au haifai.

“Hii pia itatoa nafasi kwa wataalamu wetu kuwa sehemu ya mjadala wa tiba ya Covid 19 unaoendelea kote duniani badala ya kuwa pembeni na kusubiri kila wazo au jibu kutoka kwa wenzetu. Na hii pia inawakumbusha wataaalamu wetu kwamba tunachokikubali kuwa ni njia sahihi kimeanza kwa namna hii na watalaamu wetu wawe tayari kufanya utafiti na kuchangia kutoa majibu yanayohitajika badala ya kusibiri kila kitu tufanyiwe na kuletewa mezani.”

Aidha, MHN imeeleza kuwa mpaka sasa zaidi ya wananchi 1,100 wakiwemo wataalamu wa afya (madaktari, wauguzi n.k) waliotumia huduma hiyo wametoa taarifa ya kuridhishwa nayo.

“Sasa ni muhimu wataalamu wetu wa design study ambayo itatupa majibu sahihi,” imeeleza taarifa hiyo.

“Aidha Hospitali ya Taifa Muhimbili yenye dhamana ya kutoa elimu, kutibu na kufanya utafiti itakua inatimiza malengo na majukumu yake, kwa muktadha huu MNH, haitaondoa huduma hiyo kwa kuwa iko kwenye utekelezaji sahihi wa majukumu yake ya kitafiti kama wanavyofanya wanasayansi wengine kote duniani, ” imehitimisha taarifa hiyo.

TCRA: Vifurushi vya zamani vitarejea ndani ya siku 4
Algeria: Upinzani watangaza kususia uchaguzi wa Bunge