Rais, Dkt. Joh Magufuli amehutubia Taifa leo na kutoa taarifa kuhusu virusi vya Corona vilivyoingia nchini ambapo amesema hadi sasa kuna wagonjwa 12.

Rais Magufuli amesema hayo baada ya kujumuika na Waumini wengine wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu la Dodoma katika Ibada iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Onesmo Wissi.

Amesema “Kamati ya Kupambana na Ugonjwa huu imeiimarishwa na sasa itakuwa chini ya Waziri Mkuu akishirikiana na Waziri wa Afya. Wageni wote kutoka kwenye mataifa yalioathorika zaidi watatakiwa kukaa Karantini kwa siku 14 kwa gharama zao”

Akizungumza maendeleo ya afya za wagonjwa walioathirika Rais Magufuli ameufahamisha umma kuwa mpaka leo Machi 22, 2020 Tanzania ina wagonjwa 12 ambao wote wanaeendelea vizuri na matibabu yao ambapo Mgonjwa wa kwanza kutangazwa nchini amepimwa na kukutwa hana maambukizi tena.

Amesema kuwepo kwa homa ya corona nchini isiwe sababu ya kutishana kiasi cha kumsahau Mwenyezi Mungu, hivyo ametoa wito kwa Waumini wa dini ya Kikristo na wale wa madhehebu mengine nchini kumrudia Mwenyezi Mungu ili aliepushe Taifa na virusi hivyo.

Rais Magufuli amekemea tabia za baadhi ya watu wanaofanya mzaha juu ya homa ya corona ama kuwatia hofu wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na badala yake ametaka Watanzania waendelee kuchapa kazi huku wakizingatia tahadhari.

“Watu tusitishane, tunatishana mno, niwaombe ndugu Wakristo na Watanzania kwa ujumla wa madhehebu yote, huu ndio wakati mzuri sana wa kumtegemea Mungu kuliko wakati wote, tuendelee kuchapa kazi, tuendelee kuujenga uchumi wetu, hatuwezi kusalimu amri kwa ugonjwa huu wa corona na kushindwa kumtegemea Mungu na tukashindwa kuendeleza uchumi wetu” amesema Rais Magufuli.

Amewashukuru viongozi wa dini zote nchini kwa kuungana na serikali katika kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari na ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aliepushe na homa ya corona.

Video: watakaoingia nchini sasa kutengwa, Askofu Katoliki amuwashia moto Polepole
Jinsi manjano yanavyotoa michirizi na mikunjo katika mwili

Comments

comments